Samsung Galaxy SIV imetambulishwa rasmi nchini marekani masaa machache yaliyopita jijini New York. Toleo lililopita la Samsung Galaxy SIII lilizinduliwa jijini London na kwa sasa uzinduzi huu umechukuliwa kama kuonesha ni jinsi gani soko la Marekani limekuwa muhimu kwa Samsung.
Kama kawaida yao, Samsung wameleta vitu vipya katika ulimwengu wa utumiaji wa simu katika toleo hili la Samsung Galaxy SIV.
Kwa ufupi Samsung Galaxy SIV inakuja na RAM ya GB 2, kioo (display) ya inchi tano (HD 1920 x 1080) uzito wa gramu 130, unene wa 7.9mm. Itakuwa na matoleo ya uwezo wa kuhifadhi data wa GB 16, 32 na 64, hii ni pamoja na sehemu ya kutumia ‘memory card’ (MicroSD). Inatumia Google Android 4.2.
Kitu kingine cha kipekee ni uwezo wa kamera ya nyuma, ambayo inakuja na ‘Megapixel’ 13, hii ikiwa ni moja ya uwezo mkubwa sana wa kamera za simu (Galaxy SIII ilikuwa na kamera ya megapixel 8). Pia ina kamera ya mbele ya megapixel 1.9.
Rasmi Galaxy SIV Inakuja Na Rangi Mbili, Nyeupe na Nyeusi. |
Teknolojia tatu muhimu katika kuboresha furaha katika utumiaji ni kuja kwa ‘Smart Pause’, ‘Smart Scroll’ na ‘Air View’. Smart Pause na Smart Scroll ni teknolojia zitakazomuwezesha mtumiaji kuitumia simu yake kupitia kupepesa macho yake akiwa anakiangalia kioo cha simu, kazi hizi ni kama kusimamisha video, na pia kushusha na kupandisha ukurasa wa mtandao (website) unaoutumia. Air View ni teknolojia inayokuwezesha kutumia simu hii bila kuigusa bali kupitia kupunga kiganja chako. Kwa mfano unaweza kupunga kushoto au kulia unapokuwa unaziangalia picha zako, nazo zitajipitisha kulingano na upande unaopeleka mkono wako. Pia unapokuwa unatazama mtandao basi unaweza kupunga kushoto ili kurudi kwenye ukurasa uliopita na kupunga kulia ili kwenda ukurasa wa mbele. Unaweza pia kupunga ili kupokea simu, hizi ni baadhi tuu ya vitu unavyoweza fanya kupitia hizi teknolojia mpya.
Samsung Galaxy SIV itaingia rasmi sokoni muda wowote sasa, Samsung bado hawajatangaza tarehe rasmi ambayo simu itapatikana madukani, pia ata bei bado haijatangazwa. Kwa sasa tutasubiri kuona kama Galaxy SIV itafikia mafanikio ya Samsung Galaxy SIII ambayo ni moja ya simu zilizouza zaidi duniani. iPhone 5S ipo njiani hadi hapo tutaona kama itafikia hadhi ya Galaxy SIV ingawa watafiti wengi wanasema inaweza ikawa vigumu.
No Comment! Be the first one.