Kuna kipindi ilikuwa kwamba ukisikia skrini (kioo) basi mawazo yako yanapata taswira ya kitu kikubwa na chenye mwinuko fulani nyuma yake (kisogo). Miaka imeenda na teknolojia ya skrini haijabaki nyuma. Skrini za kisasa ni nyembaba, nyepesi na zinapatikana kwenye vifaa vingi vya majumbani na kazini. Kwa upande wa simu, na hata luninga kwa sasa teknolojia za skrini zinazotamba ni LCD na OLED. Tuzichambue.
TFT-LCD
Teknolojia inayotumika zaidi kwenye simu za mkononi ni Thin-Film Transistor Liquid Crystal Display (TFT-LCD) ambayo watu wengi huifupisha kuwa LCD tu. Hii ni kwa sababu kuna aina nyingi za LCD ila kiuhalisia aina ya TFT ndiyo inayotumika zaidi. Unaweza kuiona LCD kwenye simu za hali zote – za hali ya chini, kawaida kama HTC Desire C na hata za hali ya juu zaidi kama iPhone. Kwa mantiki hiyo kujua tu kwamba simu flani ni LCD hakuwezi kukupa picha ya kiwango cha skrini yake, kwani tayari tushasema kuna aina tofauti na namna kadhaa tofauti za kutengeneza LCD ambazo makampuni tofauti yanazitangaza kwa majina tofauti ya kimauzo kwa mfano Retina Dislay, PureMotion na kadahalika.
Skrini za LCD hutengenezwa kwa material yenye tabia za chembe za kioevu na chembe imara (‘liquid and solid atoms’) na zinahitaji kumulikwa ili iwake. Umeme ukipitishwa kwenye kioo cha LCD, unasababisha mwanga kupita katikati ya pixeli na kutoa rangi. Kwenye skrini za rangi tofauti, kila pixeli hugawanywa katika rangi tatu – nyekundu, bluu na kijani. Ukiangalia kiundani sana kwenye kioo kama hiki utaweza kuona huu mgawanyiko.
Kwa kawaida, kioo LCD kwenye simu ya bei nafuu huwa na rangi hafifu na inaweza kuonekana kwa ‘angle’ ndogo sana. Hii inamaanisha ukiangalia kipembeni kidogo, inakuwa ngumu kuona vizuri kilichopo kwenye skrini. Kioo cha simu ya hali ya juu huwa na rangi ng’aavu, za kihalisia na uwezo wa kuonekana kwa ‘angle’ yoyote.
Kioo chochote cha LCD kinahitaji kumulikwa na taa – kwa mfano ‘tube-light’ ndogo kabisa utakazoziona unapofungua simu na kuchunguza kioo chake. Hii ndio sababu inayozifanya simu zenye LCD kuwa kubwa kidogo kulinganisha na zile zenye teknolojia nyingine ya OLED. Na kwasababu hii pia, rangi nyeusi kwenye vioo vya LCD haiwi nyeusi kabisa, inakuwa na upaukaji kidogo na pia huwa zinatumia chaji nyingi zaidi. Kinachoweza kuvutia labda kwenye teknolojia hii ni unafuu kwenye utengenezaji wake na ndio maana kampuni nyingi huitumia teknolojia hii. Mfano mzuri ni miaka ya nyuma kidogo wakati HTC walipositisha matengenezo ya HTC Desire iliyopangwa kuwa na kioo cha OLDE na kuamua kutumia LCD.
Retina Display ni teknolojia ya Apple na ni mojawapo ya aina za LCD iitwayo In-place Switching (IPS). Teknolojia hii inatofautishwa na aina nyingine za LCD kwa ujazo wa pixeli. Apple wanasema ujazo wake ni mkubwa zaidi ya uwezo wa jicho la binadamu kupambanua kati ya picha ya skrini na kitu cha ukweli. Hata hivyo, huu ni mfano wa jinsi kampuni inavyoweza kutofautisha teknolojia yake. iPhone 5, iPad Air, na pia Google Nexus 5 zote ni mifano ya simu zinazotumia skrini za LCD.
OLED
Active-matrix Organic Light-emitting diode, au AMOLED kwa kifupi, ni teknolojia ya vioo inayotengenezwa kwa misombo ya kikaboni (‘organic compounds’). Vioo hivi vina sifa ya kuonesha picha zenye ubora wa hali ya juu kwa kutumia umeme mdogo zaidi.
Tofauti na vioo vya LCD, vioo vya AMOLED hazihitaji kumulikwa – kila pixeli hutoa mwanga wake wenyewe na kwa sababu hiyo, simu zinaweza kuwa nyembamba zaidi. Uwezo huu wa kujimulika unamaanisha pia kwamba kwenye vioo vya teknolojia hii, nyeusi huwa nyeusi kweli kuliko vile ilivyo kwenye LCD. Pamoja na hili, teknolojia ya OLED inajulikana kwa kuonesha video vizuri kuliko LCD kwani ‘refresh-rate’ yake ni ya haraka zaidi.
Pamoja na manufaa yake, utengenezaji wa vioo vya AMOLED huwa wa gharama zaidi na ni teknolojia hii ni ngumu zaidi kutengeneza kwa wingi kuliko LCD, kitu ambacho kilifanya utengenezaji wa HTC Desire usimame katikati na kubadilishwa vioo kuwa Super-LCD.
AMOLED ina mpangilio wa vi-pixeli tofauti na LCD, ambao unaweza kufanya picha kuwa tofauti na ule wa LCD. Pia, imejulikana kwamba kwenye vioo vya AMOLED rangi ya bluu hufifia haraka zaidi kuliko rangi zingine, na hivyo kuathiri uwiano wa rangi kadri simu inavyozidi kuzeeka. Unaweza kuona kioo cha aina ya OLED kwenye simu za LG G Flex na Samsung Galaxy Round.
Samsung nyingine kama Galaxy S5, zina Super AMOLED screens, zinazotumia teknolojia ya AMOLED pamoja na ‘capacitative touch-screen’ kufanya simu kuwa nyembamba, nyepesi na zenye uhalisia zaidi. Pia, kutokana na sifa za OLED, inawezekana kutengeneza vioo vinavyoweza kukunjwa kama vile kwenye simu ya LG-Flex na baadhi ya luninga za kisasa zaidi.
Ipi Zaidi?
Unaponunua simu, kuna mambo mengi utaangalia. Kioo cha simu kinaweza kisiwe sababu kuu ya kuchagua simu, ila ubora na teknolojia yake ni jambo muhimu unalopaswa kueliewa ili mategemeo yako yawe na uhalisia. Pia, unaposikia kwamba iPhone ina Retina Display, Samsung ina Super-AMOLED au Lumia ina PureMotion HD+, haya ni majina tu ya kimauzo yanayotumiwa na makampuni kutangaza biashara yake. Hii haimaanishi kwamba majina haya hayana uhalisia, ila tu rejea tena, ni muhimu kujua yana maana gani kiteknolojia.
Usisite kuwasiliana nasi. Endelea kufurahia habari, uchambuzi na makala za teknolojia hapa teknokona.
No Comment! Be the first one.