Wakati Matangazo ya Televisheni yalipoanza nchini Tanzania, watu wengi walikuwa wakipatwa na mshangao kwa wasomaji wa Taarifa ya habari namna walivyokuwa wakisoma habari bila ya kuangalia kwenye karatasi.
Wengi hawakujua ni teknolojia gani inayotumika na wengine kuamini watangazaji walikuwa wamekariri.
Wengi walisumbuka kujua nini kilikuwa kikiendelea. Lakini si hao tu hivi karibuni kumetokea tena ubishani unaofanana na huo. Huu ni pale viongozi wa kitaifa wanapohutubia hotuba ndefu na kutoonekana kusoma popote.
Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho kikwete kwa mara ya kwanza alipohutubia bunge mwaka 2005 hakuonekana kushika karatasi na alitoa hotuba ya karibu saa moja na nusu. Hatua hiyo iliwachanganya wengi akiwemo Mbunge wa Bariadi wa wakati huo John Momose Cheyo.
Cheyo alipokuwa anatoa maoni yake kuhusu hotuba ya Rais, mwisho alimsifia kwa kuweza kuzungumza hotuba yote bila ya kusoma sehemu yoyote. Sio Cheyo tu watanzania wengi walimsifia Rais kwa kuzungumza Hotuba ya Dakika 90 bila ya kusoma sehemu yoyote.

Ukweli ni kwamba Watangazaji wa habari wa televisheni husoma na viongozi wa kitaifa pia husoma hotuba zao.
Nini kinachofanyika? Ni teknolojia ya Teleprompta (Teleprompter)
Teleprompta ni nini?
Ni kifaa maalumu ambacho kinamsaidia mtu kusoma maandishi yanayoonekana katika kioo kilichopo katika kifaa hicho.
Ndani yake huwekwa Programu maalumu inayowezesha kuingia Data zitakazowekwa na kusomwa na muhusika katika kile alichokusudia kusoma.
Teleprompta inatumiwa na viongozi wengi, wasanii katika fani ya maigizo hususani wale wenye script ndefu na wasomaji habari katika vituo vya Televisheni. Kwa ufupi inatumika kusoma maandishi kama hotuba, habari nk.

Kwa upande wa muhusika (anayesoma) yeye anaona maandishi yanapita na kumuwezesha kusoma kilichoandikwa. Ukikaa upande wa watazamaji hauoni hayo maandishi, utaona kioo ni cheupe kisicho na chochote.
Jina la Teleprompta linatokana na Kampuni ya TelePrompTer Corporation ya huko Marekani inayokadiriwa kuanzishwa mwaka 1950 mpaka 1981 na Mfanyabiashara Irving B. Kahn pamoja na wenzake wengine.
Rais wa kwanza wa Marekani kutumia Teleprompta alikuwa ni Dwight Eisenhower mwaka 1954. Kwa Tanzania Rais wa kwanza kutumia alikuwa ni Jakaya Kikwete pale alipohutubia Bunge la Tanzania mwaka 2005.


Teknolojia ya Teleprompta inapotumika kwa Marais kutoa hotuba zao hutumika mbili. Moja upande wa kulia na nyingine upande wake wa kushoto.
Hufanyika hivi ili iwe rahisi kwa Rais kuangalia pande zote za wasikilizaji wake bila ya kuonekana Rais anatoa hotuba kwa kuangalia upande mmoja wa wasikilizaji.
Teknolojia hiyo imekuwa zaidi kwa sasa mtu anaweza kutumia Tablet/Ipad kusoma hotuba ni kiasi cha kuweka App maalumu.