Katika matoleo ya simu, kampuni huweka umakini mkubwa katika toleo kubwa zaidi, kulijaza na sifa nyingi ambazo ndizo bora kwa wakati huo, ili kuifanya simu hiyo kuonekana bora zaidi ya ushindani. Kwa sasa, toleo hilo kwa kampuni ya Xiaomi ni simu yao ya Xiaomi 12S Ultra, ikiwa imejazwa sifa mbalimbali mbazo ndizo bora kwa ulimwengu wa teknolojia kwa sasa.
Kwa kuanzia, skrini ya simu hii ni moja kati ya skrini bora za simu duniani, yenye ukubwa wa inchi 6.73, ikitumia paneli ya AMOLED yenye ubora wa hali ya juu, na teknolojia ya LTPO 2 ambayo inaruhusu kuongeza ama kushusha kasi ya kuonekana kwa taarifa (Refresh rate) ili kuboresha matumizi ya simu husika.

Kamera ni sehemu nyingine ambapo Xiaomi wameboresha katika simu hii, na ndio eneo kubwa zaidi lililowekewa umakini katika simu hii. Hata mwonekano wa simu unaweka wazi kabisa, kwa kuitazama tu, namna ambavyo Xiaomi wamelenga simu hii kupiga picha bora zaidi kuliko simu nyingine.
Xiaomi wameshirikiana kwa ukaribu na kampuni za Leica na Sony katika kuhakikisha wanatengeneza simu yenye camera bora, wakitumia sensa kubwa zaidi iliyotengenezwa maalumu kwa ajili ya simu aina ya Sony IMX989, sensa yenye ukubwa wa inchi 1* yenye uwezo wa Megapixel 50, ambayo Xiaomi wanasema, ina uwezo wa kupiga picha zenye uhalisia zaidi, kutokana na ubora wake, pia na mfumo wake wa matumizi uliofanyiwa kazi kwa kushirikiana na kampuni ya Leica ili kuonesha uhalisia zaidi, na kumpa mtumiaji wa simu hiyo uhuru wa kuchagua mitindo mbalimbali ya picha pamoja na video. Kuna kamera mbili Zaidi nyuma, kila moja ikiwa na uwezo wa Megapixel 48, na kamera ya mbele ikiwa na uwezo wa Megapixel 32.
Simu hii inatumia Chipset  aina ya Qualcomm Snapdragon 8+ Gen 1, ikiwa ndio bora zaidi kwa sasa katika simu za Android, huku ikiwa na RAM ya GB 8 ama 12, na uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu wa GB 256 au 512. Inakuja na mfumo wa Android 12, ukiwa na mwonekano wa MIUI 13 uliobuniwa na Xiaomi.
Simu hii ina betri yenye ukubwa wa 4860 mAh yenye uwezo wa kuchaji kwa waya kwa nguvu ya Watt 67, ikijaa toka asilimia 0 mpaka 100 kwa dakika 41, uwezo wa kuchaji bila waya kwa nguvu ya Watt 50, ikijaa toka asilimia 0 mpaka 100 kwa dakika 52 na uwezo wa kuchaji vifaa vingine bila waya (Reverse Charging) kwa nguvu ya Watt 10.
Simu hii ina teknolojia ya utambuzi wa alama za vidole katika skrini, ikitumia waya wa kuchaji na taarifa aina ya USB Type-C. Haina sehemu ya kuchomeka earphones. Pia ina teknolojia za kisasa za mawasiliano, ikisapoti mawasiliano kwa kasi ya 5G, pamoja na huduma za WiFi 6e pamoja na Bluetooth 5.2
Xiaomi 12S Ultra ina matoleo mawili ya rangi, Nyeusi na Kijani. Itauzwa kuanzia Euro 950 (Takribani Tshs 2,216,500)*
*Kipimo cha sensa ya kamera cha inchi 1 si kwa ukubwa halisi wa sensa, bali ni tafsiri katika teknolojia ya upigaji picha. Teknolojia hiyo itaelezewa zaidi katika makala tofauti.
*Bei hiyo ni kutoka nchini China. Bei katika nchi nyingine yaweza kuwa tofauti kutokana na tozo za kodi pamoja na usafirishaji.
No Comment! Be the first one.