Microsoft wameendelea kufikia tamati ya vitu vyao vya zamani na safari hii ni zamu ya programu endeshi nyingine kwa maana ya kwamba mmikiki ataacha kutoa ulinzi kwenye Windows 7.
Utakumbuka kuwa hii sio mara ya kwanza kwa wahusika kuamua kitu kama hicho kwani ilikuwa vivyo hivyo kwa Windows XP mwaka 2014. Masasisho yenyewe yanapatikana kwa baadhi ya walengwa tena kwa kulipia.
Kampuni/taasisi zinazotumia Windows 7 kwenye kompyuta zao watalipia ili kupata msaada wa kiusalama kwenye programu hiyo mpaka mwaka 2023 na baada ya muda huo mambo yatafikia mwisho kwa wote.
Ada za kupata masasisho hayo hazitakuwa zinafanana kuanzia mwaka 2020-23 bali zitakuwa zikipanda mwaka hadi mwaka mpaka hitimisho rasmi la kutoa masasisho litakapofikiwa.
Ili kufanikiwa katika jambo fulani ni muhimu kutumia mbinu mbalimbali sasa Microsoft wametumia namna fulani ya kuongeza mauzo ya Windows tena; utalazimika kuboresha kutoka Windows 7 mpaka Windows 10 na mwisho wa siku idadi ya watumiaji itaongezeka.
Kama ulikuwa hufahamu fahamu sasa kwamba Windows 7 haina hata muongo mmoja tangu kuanza kutumiwa; ilizinduliwa mwaka 2009.
Vyanzo: Engadget, Tech Times