Watafiti wagundua Apple ipo njiani kufanya ubadilishaji wa betri za iPhone kwa mafundi wanaojitegemea kuwa jambo gumu, ikiwa ni njia ya kulazimisha ufundi huo kufanywa kupitia maduka yao spesheli, yaani Apple Stores.
Kampuni maarufu ya utafiti wa matengenezo ya iFixit imetoa ripoti inayoonesha kwenye simu mpya za iPhone XR, XS na XS Max kama betri likibadilishwa kupitia matengenezo binafsi basi ingawa simu itawaka kama kawaida ila kuna ujumbe utakuwa unatokea kila saa ‘unable to verify this iPhone has a genuine Apple battery’ – simu itakuambia inashindwa kuhakiki kama simu yako ina betri sahihi kutoka Apple. Pia hii inamaanisha hautapata tena taarifa zinazohusu hali ya ubora wa betri – ‘battery health’.

Inasemekana Apple wamekuja na mfumo unahusisha teknolojia ya kuunganisha uhusiano kati ya simu na betri lake, na kupitia teknolojia hiyo ndio pia taarifa za hali ya betri zinaweza kusomwa na simu yako kupitia kipengele cha ‘battery health’ yaani afya ya simu.
iFixit wamesema suala hilo wamegundua linatokea ata kama utatumia betri orijino la Apple, njia pekee ya kuweka mambo sawa ni kwa kupeleka simu hiyo kwenye maduka spesheli yanayotambulika na Apple – Apple Store. Inaonekana kuna programu wanayotumia kuifanya simu yako na betri kuwa na uhusiano wa kutambuana.
Watu wengi wamechukizwa na jambo hili kwani kwa namna moja linaonesha Apple wanataka kuzidi kulazimisha watu kutumia maduka yao kwa matengenezo – bei/gharama za matengenezo katika maduka haya huwa ni juu ukilinganisha na mafundi wengine.
Tayari makundi ya watumiaji mbalimbali wa vifaa vya elektroniki nchini Marekani wameanzisha harakati za kuomba sheria ya kubana makampuni kama Apple kulazimisha watu kufanya matengenezo kwa kuwategemea wao tuu. Harakati hizo zinatambulika kwa jina la ‘Right to repair’, yaani haki ya utengenezaji. Watumiaji wanadai kwa kununua kifaa wanatakiwa wawe na haki ya kufanya matengenezo yeyote bila kulazimika kurudi kwa mtengenezaji.