Wiki ya ubunifu (Innovation Week) chini ya udhamini wa HDIF inaendelea jijini Dar es Salaam. Na leo nitakueleza kuhusu teknolojia iliyonivutia. Leo fahamu kuhusu Tungulizibomba! 🙂
Kupitia shunguli hii utaweza kujionea teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na kutengenezwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kijamii – katika kutatua matatizo au changamoto mbalimbali zilizopo sehemu mbalimbali nchini.
Tungulizibomba ni vifaa vya kudhibiti mbu ambavyo husimikwa kwenye sehemu ya juu kabisa ya ukuta iliyokaribu na paa la nyumba ‘tungulizi’. Ndio mara yangu ya kwanza kuliona neno hili na uhakika kwa wengi wetu itakuwa ni mara ya kwanza pia.
Kukusaidia kuelewa maana ya Tungulizi.
Kama umeona nyumba za matofali ya kuchoma au udongo utakuwa unagundua ya kwamba kuna matundu huwa yanachwa wazi eneo la juu la kuta za nyumba hizo, karibu na eneo la bati. Matundu hayo ndio yanaitwa tungulizi, na hivyo vifaa hivyi vya kuwekwa eneo hilo kwa ajili ya kudhibiti mbu vimepewa jina la Tungulizibomba.
Ufanyaji kazi wa Tungulizibomba

- Tungulizi iliyo wazi huwekwa tungulizibomba na kisha kuzibwa sehemu zilizo wazi.
- Tungulizi iliyozibwa hutobolewa matundu na kuwekwa tungulizi bomba.
- Kiasi kikubwa cha harufu ya binadamu hutoka nje kupitia tungulizibomba na kisha kuvutia idadi kubwa ya mbu wa Malaria.
- Wakati wa kuingia kwenye tungulizibomba, mbu hugusana na kipande cha neti kilichotiwa dawa na kufa papohapo au muda mfupi baadae.
Faida za teknolojia hiyo

- Ni rahisi kutumia
- Inaua kwa haraka hata pale mbu wanapogusana na dawa kwa muda mfupi
- Ina uwezo wa kuua hata mbu waliojengwa usugu dhidi ya dawa za kuulia mbu zinazotumika kwa sasa
- Inakinga familia nzima ndani ya nyumba
- Ni rafiki wa mazingira kwa kuwa inatumia kiasi kidogo cha dawa na neti ikilinganishwa na teknolojia nyingine
Teknolojia hii imegunduliwa na watafiti mbalimbali wakiwa chini ya programu ya MCD (Mosquito Contamination Device), programu iliyochini ya udhamini wa Umoja wa Ulaya ikiwa imejikita katika teknolojia za kupambana na Mbu na Malaria.