Kwa sasa kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia inaonekana kuzidi mno katika kila nyanja ili kurahisisha maisha ya mwanadamu.
Pamoja na kukua huko lakini kuna hatari ya kupunguza ajira za watu wengi makazini. Huko nchini Uturuki tayari wamezindua usafiri wa treni ziendazo kasi na zisizotumia Dereva. Zinajiendesha zenyewe.

Meya wa jiji la Istanbul Kadir Topbaş amesema kwamba treni za kasi 8 maarufu kama metro zisizokuwa na dereva zimeanza kutumika katika jiji hilo kubwa zaidi nchini Uturuki.
Metro hizo zimeanza kutoa huduma ya usafiri ndani ya jiji hilo kutoka Hacıosman mpaka Yenikapı eneo lenye umbali wa kilomita 23.5.

Treni hizo za kasi zitaweza kubeba takriban abiria 350, 000 kila siku. Treni zingine jumla ya 60 zitaanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu.
Meya Topbaş alikuwa anaongea siku ya jumamosi katika hafla jijini humo na kufahamisha kwa metro hizo 68 zisizo na dereva zitarahisisha usafiri pamoja na 92 ambazo huendeshwa kwa kutumia dereva nchini humo.