Kama umekuwa ukifuatilia teknlojia, wiki hii kumekuwa na gumzo kubwa mtandaoni kufuatia maonesho ya CES2015. CES, yani kifupi cha ‘Consumer Electronics Show’ ni maonyesho ya kimataifa ya teknolojia inayomlenga mtu wa kawaida yanayofanyika kila mwanzo wa mwaka huko Las Vegas, Marekani.
Maonyesho hayo yanavutia kampuni mbalimbali vinara za teknolojia duniani ambao wamekuwa wakitumia maonyesho hayo kutangaza teknolojia zao mpya kama ilivyo kwa Microsoft na XBox mwaka 2001, Google na Android (2010) na magari yanaojiendesha (2013).
Mwaka huu, ushindani mkubwa unaoongelewa na wengi katika maonesho ya CES ni wa TV za teknolojia mpya iliyopewa jina la ‘4K technology’. 4K inamaanisha uhalisia wa picha mara 4 zaidi ya picha za teknolojia ya HD. Kampuni za Korea ya Kusini, Samsung na LG ndio wapinzani wakubwa katika soko la TV za kisasa.
Samsung wanatamba na teknolojia wanayoiita ‘SUHD’, yani Samsung ‘Ultra High Definition’ wakati LG wakijigamba kwa kuwa kampuni pekee ilyofanikiwa na ‘OLED’, teknolojia amabayo inaonesha picha yenye uhalisia zaidi huku ikitumia umeme mdogo zaidi ya teknolojia pinzani. Ukiachana na teknolojia ya 4K, TV za aina mbalimbali zimetambulishwa zikiwemo TV za mkunjo na TV nyembemba kuliko iphone, zinazotengenezwa na Sony – Sony Bravia X900C.
Samsung wamefunika wakitamka kwamba ifikapo mwaka 2017 hawatatengeneza tv zisizokuwa na uwezo wa intaneti. Hii ni ishara kubwa inayoonesha kwamba soko linaelekea kwenye teknolojia za intaneti ya vitu (Internet of things).



Kutokana na tamko hilo la Samsung, mategemeo ya wachambuzi wengi wa mambo ya teknolojia na maonesho mbalimbali kwenye CES2015, mwaka huu unategemewa kuona teknolojia hizi intaneti ya vitu ikiendelea kukua kwenye nchi zilizoendelea . Wachambuzi wanatazamia kwamba kuna kipindi karibu kila kitu cha kielektroniki tunachotumia kitakuwa kimeungwa na mtandao wa intaneti.
Teknolojia kama hizi ambazo zimepata vichwa vya habari katika CES mwaka huu ni kama teknolojia ya kunyonyesha watoto, teknolojia ya pedali za baiskeli, teknolojia ya pete inayofanya vitu mbalimbali kama kufunga mapazia na hata teknolojia inayoongeza ukubwa wa mkanda baada ya kula mlo mkubwa.
Teknolojia ya magari yanayojiendesha inakuwa zaidi kwani tayari makampuni mbalimbali ya magari ikiwemo Audi na Mercedes Benz wameonesha aina kadhaa ya magari ya aina hiyo kwenye maonyesho ya CES mwaka huu. Ni dhahiri teknolojia hii itazidi kukua na muda si mrefu mambo kama haya yatatiririka kwenye bara la Afrika.





No Comment! Be the first one.