fbpx
TeknoKona Teknolojia Tanzania

Intaneti Tanzania Teknolojia

Tanzania Inaongoza kwa bei nafuu katika huduma ya intaneti Afrika- ‘Ripoti’

Tanzania Inaongoza kwa bei nafuu katika huduma ya intaneti Afrika- ‘Ripoti’

Je unalalamika ya kwamba bei za vifurushi vya data vipo juu sana? Unaweza ukawa unakosea, ripoti moja inaonesha Tanzania inaongoza kwa bei nafuu zaidi katika huduma ya intaneti barani Afrika.

Uwepo wa watoa huduma wengi uleta ushindani na pia unachangia uwepo wa bei nafuu pia.

Hadi sasa hatujafanikiwa kuipata ripoti nzima ila vyombo vya habari vilivyofanikiwa kuisoma ripoti hiyo iliyotolewa Afrika Kusini inaonesha watumiaji intaneti wa Tanzania ndio wanaonufaika kwa bei nafuu zaidi.

Wastani wa bei ya GB 1 ni dola 0.89 ya Marekani, (kumbuka Dola 1 = takriabni Tsh 2200) unaifanya gharama ya huduma hii kuwa chini sana ukilinganisha na mataifa mengine kama vile;

  • Afrika Kusini – Dola 5.26 kwa GB 1
  • Kenya ni Dola 5.0 kwa GB 1
  • Misri ni Dola 2.8 kwa GB 1
  • Naijeria ni Dola 5.26 kwa GB 1
  • Malawi ni Dola 5.8 kwa GB 1.

Tofauti ya bei ni kubwa sana. Kwa muda mrefu tumekuwa tukifahamu ya kwamba bei za huduma za intaneti Tanzania ni nafuu lakini ripoti inaonesha kiwango cha unafuu ni kikubwa kuliko tulivyokuwa tukidhani kabla.

Watumiaji wa huduma za intaneti katika nchi zingine barani Afrika ukiwaambia kuhusu vifurushi kama vile vya UNLIMITED vya 4G LTE kutoka mtandao wa SMART kwa Tsh 69,900/= kwa mwezi watakuona unatania..

SOMA PIA  Majaribio ya makazi ya kujazwa upepo katika anga yakwama!

Kwa nini bei ni nafuu Tanzania?

  • Suala la unafuu linakuja kutokana na mambo mengi hii ikiwa ni pamoja na unafuu wa miundombinu, hasa hasa kwa uwepo wa mikongo ya intaneti ya kasi iliyounganishwa na mabara mbalimbali kama vile SEACOM. Na usambazaji wa mikongo hiyo ndani ya nchi kufikia maeneo mbalimbali na hivyo kufanya gharama za uunganishaji wa huduma hiyo kwa minara ya simu kuwa nafuu.
  • Pia kuna suala la ushindani. Tanzania hakuna mtandao mmoja wa simu unaomiliki peke yako soko kwa ubavu zaidi. Ukiangalia mataifa mengine kama vile Kenya ambapo mtandao wa simu wa SafariCom unamiliki soko kwa asilimia kubwa sana (Chanzo: Techweez – ) hili linafanya ushindani wa kibei kuwa mgumu kidogo. Uwepo wa mitandao mingi Tanzania unasababisha ushindani mzuri unaohusisha hadi bei na hivyo watumiaji ndio tunaonufaika zaidi.
  • Kingine ni serikali. Iwe isiwe ni lazima kuishukuru serikali yetu katika hili kwani kama kungekuwa na tozo na kodi nyingi sana katika sekta hii basi hadi bei ya huduma ingekuwa juu.

Watumiaji wa Afrika Kusini wadai ushushwaji wa bei!#DataMustFall

Ripoti hiyo ya ICT Africa inaonesha kwa wastani mwananchi wa kawaida wa Afrika Kusini anatumia asilimia 20% ya pato lake kwa mwezi kutumia GB 1 ya intaneti!

Kuna kampeni kubwa ya watumiaji wa huduma ya intaneti Afrika Kusini imeanzishwa. Lengo kuu ni kulazimisha mitandao ya simu ya nchini humo kushusha gharama zao za huduma ya intaneti. 

Kampeni hiyo inayotrend hadi Twitter kwa hashtag ya #DataMustFall imeipa mitandao ya simu nchini humo siku 30 za kushusha gharama za huduma hiyo wakidai gharama ya sasa hivi ni sawa na ujambazi. Kumbuka kwa wastani inawagharimu zaidi ya Tsh 12,000/= kwa kila GB 1!

Wewe unatumia mtandao gani na huwa unatumiaga kifurushi gani cha data na kwa bei gani? Je unaona ni nafuu?

Kumbuka kusambaza makala na pia kuungana nasi kupitia Facebook, Twitter, Instagram, YouTube, Telegram na Google Plus

Vyanzo: CCTV-Afica, na vyanzo mbalimbali

Comrade Mokiwa

Comrade Mokiwa

Muanzilishi wa Teknokona na Teknokona Group LTD - WWW.TEKNOKONAGROUP.COM

Muda wangu umegawanyika kati ya kazi kibunifu @teknokonagroup na uandishi wa habari za Teknolojia hapa Teknokona Blog.

| mhariri(at)teknokona.co.tz |

Comment

TeknoKona Teknolojia Tanzania