Watafiti wa mambo ya usalama wa mitandao wamegundua makosa katika protokali ya WPA2 ambayo imekuwa ikitumika katika WI-FI.
Makosa haya yanapelekea wadukuzi kuwa na uwezo wa kuingilia mawasiliano baina ya kifaa kinachorusha wi-fi na kifaa kinachopokea. Kwa kutumia mwanya huu uliogundulika wadukuzi wanaweza kupata taarifa mbalimbali za mtu anayetumia mtandao kupitia WiFi husika, taarifa hizi zinaweza kuwa ni barua pepe na pia nywila ambazo mtumiaji alitumia kufungua mtandao.
Watafiti hao Mathy Vanhoef na Frank Piessens wameonesha na kuthibitisha utafiti wao ambao umechapichwa katika jarida la mtandaoni, katika video hiyo Mathy anaonesha jinsi mdukuzi anavyoweza kuchukua taarifa za mtumiaji aliye katika WiFi ambayo inatumia protokali za WPA2.
Itazame video ya watafiti hao wakionesha namna watumiaji wanavyoweza kudukuliwa
Ingawa vifaa ambayo vinatumia Android pamoja na vile vinavyotumia Linux ndio viko katika hatari zaidi ya kushambuliwa (hii inatokana na kosa dogo katika programu ya WPA2 ya vifaa hivyo) lakini bado tatizo hili ni kubwa kwa kuwa kwa asilimia fulani kila kifaa kinachotumia WiFi kitashambuliwa.
Apple wamesema tayari sasisho (update) jipya lipo la kuondoa kabisa mwanya huo wa udukuzi, ila kwa vifaa vya Android – simu nyingi zitakuwa kwenye hatari kwani masasisho uchukua muda mrefu kuwafikia watumiaji na mara nyingi simu nyingi huwa hazijayapati.
Tayari kuna jitihada zinafanywa na watengenezaji wa vifaa vya WiFi kuweza kurekebisha tatizo hili lakini utatuzi wa tatizo hili utahusisha usasishaji wa programu za vifaa hivyo.

Kwa Tanzania tatizo hili litakuwa kubwa kuliko sehemu ambazo teknolojia imeendelea zaidi, hii ni kwasababu makampuni mengi ambayo yanatoa huduma hizi hayatajisumbua kubadili vifaa ama kusasisha vifaa wanavyotumia.