SpaceX na rekodi za Anga, inaendelea kuweka rekodi za kitofauti na za kipekee katika usafiri wa anga za juu, safari iliyopewa jina Polaris Dawn imezidi kuwaweka kama kampuni ya mfano katika safari za anga.
Safari ya kwenda anga ya juu kutoka uso wa dunia, eneo lenye mionzi mikali (radition) ya jua, ilizinduliwa mnamo Septemba 10, 2024, ilikuwa na malengo kadhaa ya kukagua ubunifu na uwezo wa teknolojia za SpaceX katika safari za Anga zinazohusisha kwenda safari za mbali nje ya eneo linalozungukwa na satelaiti mbalimbali hii ikiwa ni pamoja na Stesheni ya Kimataifa ya Anga za Juu. Safari hiyo imekamilishwa kwa kifaa kutua kikiwa na wanaanga wake mchana wa Septemba 15.
Rekodi Muhimu na Mafanikio yaliyofikiwa:
1. Safari ya Kwanza ya Kibinafsi ya Kutembea Angani:
Polaris Dawn imeweka historia kwa kuwa ni safari ya kwanza ya kampuni binafsi kuwezea kuwezesha wanaanga kutembea na kutoka hadi nje ya chombo cha anga. Neno maarufu likiwa ni ‘Space Walk’, yaani ni sawa wameweza kutembea huku kitu pekee kinachotenganisha anga na ngozi zao ni mavazi tuu spesheli ya mwanaanga.
2. Urefu Mkubwa Zaidi kufikiwa na Crew Dragon:
Kwenye safari hii chombo cha safari za anga cha SpaceX, chombo cha Crew Dragon kilifikia urefu wa kilomita 1,400 na hivyo kuweka rekodi mpya kwa urefu wa juu zaidi kuwahi kufikiwa na misheni ya SpaceX au kampuni binafsi inayohusisha wanaanga. Kikawaida safari zinazohusisha wanaanga huwa ni za kwenda kwenye Stesheni ya Kimataifa ya Anga za Juu, stesheni hii inaruka juu kwenye kiwango cha wastani wa km 408 juu ya uso wa dunia.
3. Suti za Kisasa za Extravehicular Activity (EVA):
Misheni hii pia imeleta suti mpya za EVA zilizotengenezwa na SpaceX. Suti hizi zimebuniwa kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusisha uwezo wa mwanaga kutembea angani, na uwezo wake wa kuweza kutumia vifaa mbalimbali kwa urahisi. Suti hizi zinaashiria hatua kubwa katika teknolojia ya mavazi ya anga, zikirahisha uwezo wa kutembea na kutumia vitu kwa urahisi, na usalama zaidi kwa wanaanga.
4. Wanaanga ‘wa kawaida’:
Misheni ya Polaris Dawn inajumuisha wanaanga, tofauti ikiwa ni pamoja na bilionea, wahandisi wawili wa SpaceX, na rubani wa kivita aliyestaafu. Tofauti hii inaonesha jinsi safari za anga zinavyozidi kufikiwa na watu wa aina mbalimbali, mmoja wa wafanyakazi wa SpaceX ni mfanyakazi aliyeanza kufanya kazi katika kampuni hiyo kama ‘intern’ tu miaka mingi nyuma.
Tafiti na Chunguzi zinazotokana na safari hii
Mafanikio ya misheni ya Polaris Dawn sio tu ni hatua muhimu kwa SpaceX bali kwa sekta nzima ya masuala ya anga za juu. Kwa kuweka rekodi mpya kwa safari za anga za kibinafsi, SpaceX inatoa mwelekeo kwa misheni zijazo ambazo zinaweza kujumuisha kutua mwezini, safari za sayari ya Mars, na zaidi.
No Comment! Be the first one.