fbpx
TeknoKona Teknolojia Tanzania

Gemu Sony Teknolojia

Sony wauza nakala milioni 100 za PlayStation 4. #Gemu

Sony wauza nakala milioni 100 za PlayStation 4. #Gemu

Spread the love

Kifaa cha kuchezea magemu cha PlayStation 4 kutoka Sony kimefanikisha kufikisha mauzo ya nakala milioni 100 tokea kuingia sokoni mwaka 2013.

Kwa mauzo hayo PlayStation 4 imechukua sifa ya kuwa bidhaa ya kuchezea magemu iliyofikia mauzo ya nakala milioni 100 kwa haraka zaidi kuliko bidhaa nyingine yeyote – hii ni pamoja na kulinganisha na mauzo ya XBOX kutoka Microsoft na pia Wii kutoka Nintendo.

Mauzo ya PlayStation 2 yaichukua miaka mitano na miezi 9 kufikia mauzo ya nakala milioni 100, wakati PS4 imechukua miaka 5 na miezi 7.

sony playstation 4

Sony PlayStation 4 – hapa ikiwa na gemu la FIFA 19, magemu ya Fifa ni moja ya magemu maarufu zaidi duniani.

Sony wanategemea kutambulisha toleo jipya la PlayStation litakalokwenda kwa jina la PlayStation 5 mwakani. Vitu vipya vinavyokuja katika toleo jipya ni pamoja na uwezo wa teknolojia ya 8K katika ubora wa muonekano – kwa sasa ni 4k, pia teknolojia ya sauti ya 3D (3D Audio), kingine ni pamoja na kuja na diski za SSD ambazo huongeza ufanisi mkubwa. Watakao kuwa na PlayStation 5 bado wataweza kutumia magamu yaliyotengenezwa kwa ajili ya PlayStation 4.

Mpinzani mkubwa wa PlayStation ni Xbox zinazotengenezwa na Microsoft. Kwa sasa Microsoft wameacha kutangaza mauzo yao ila watafiti wanasema toleo la sasa la Xbox One litakuwa limeuza nakala kati ya milioni 30 hadi milioni 60. Toleo jipya la Xbox pia litakuja mwakani na kiteknolojia wengi wanaamini teknolojia kama za 8K na diski za SSD zitatumika pia.

magemu

Soko la magemu ni kubwa kuliko ata la filamu na muziki duniani – mwaka 2018 mapato yalikadiriwa kufikia dola bilioni 137.9. Biashara ya magemu inaingia mapato makubwa zaidi, huku asilimia 50 ya mapato hayo yakitokana na uchezaji magemu kwenye simu huku mengine yakitoka kwenye magemu ya kompyuta na vifaa kama Xbox na Playstation.

Sony wamesema pia kwa sasa kwa mara ya kwanza watumiaji wake wananunua zaidi magemu kwa njia ya kidigitali – yaani kudownload kupitia mtandao kuliko kununua CD za magemu madukani. Hii inaongeza faida kwao na kwa washirika wao – watengenezaji magemu, kwani usambazaji na utengenezaji wa CD za magemu unakuwa na gharama ukilinganisha na mauzo ya kimtandao.

SOMA PIA  WileyFox: Kampuni ya simu inayotaka kunufaika na uamuzi wa Uingereza kutoka EU

Ingawa vifaa vya magemu (console) zinapata umaarufu bado soko la magemu linaongozwa kwa zaidi ya asilimia 40 na uchezaji magemu wa kwenye simu, ukifuatiwa na wa kompyuta kwa zaidi ya asilimia 25 – zinazobakia zikienda kwenye vifaa vya magemu kama Xbox na PlayStation.

Vyanzo: TheVerge na vyanzo mbalimbali
Comrade Mokiwa

Comrade Mokiwa

Muanzilishi wa Teknokona na Teknokona Group LTD - WWW.TEKNOKONAGROUP.COM

Muda wangu umegawanyika kati ya kazi kibunifu @teknokonagroup na uandishi wa habari za Teknolojia hapa Teknokona Blog.

| mhariri(at)teknokona.co.tz |

Comment

TeknoKona Teknolojia Tanzania