Kwa hakika katika teknolojia ya leo makampuni mengi yanayotoa simu janja yanaweka nguvu nyingi sana kwenye ubora wa kamera/picha ang’avu kabisa kutokana na kile kilichowekwa kwenye kamera ya simu husika.
Sony ambao wametaka kuwa mbali kabisa katika suala zima la ubora wa simu zao hasa kwenye upande wa kamera, imeingia katika historia kwa kutangaza simu yenye kamera nzuri zaidi kuliko simu janja zote duniani.
Sony IMX586 ina MP 48 huku simu janja ambazo zilikuwa zinaongoza kwa kuwa na kamera nzuri ni Huawei P20 Pro yenye MP 40 na Nokia Lumia 1020’s zina MP 41.

Sony wenyewe wanasema ubora wa picha utakuwa ni uleule hata kama mtu akijaribu kuisogeza karibu ili kuweza kuipata vizuri zaidi na ingawa hawakuionyesha simu yenye/kutoa sifa zake lakini kamera yake sio kubwa kwa umbo; ipo katika umbo la kawaida ila tu ule ubora wake kwa ndani ndio gumzo.
Sony wametumia teknolojia ya quad Bayer ambayo yenyewe kwa lugha rahisi inachuja rangi na kutumia lenzi kutoka pembe nne kuweza kupata picha bora zaidi.
Bei ya Sony IMX586 haijajulikana lakini wahusika wamesema wataanza kuzipeleka sokoni mwezi Septemba 2018. Wewe ni mpenzi wa simu janja za Sony? Basi subiri hicho kitu kipya kutoka kwao.
Vyanzo: The Verge, Gadgets 360