Simu za Huawei kukosa Google Playstore na huduma zingine za Google

Google+ Pinterest LinkedIn Tumblr +
Sambaza

Vita ya masuala ya kiusalama na biashara ya serikali ya Marekani dhidi ya Huawei inasababisha Huawei kukosa Google Playstore na huduma zingine nyingi za Google na Android  katika matoleo ya simu zake zijazo.

Ni jambo ambalo halina ubishi ya kwamba kwa miezi mingi sasa hivi tayari kampuni ya Huawei imekuwa inakula zaidi soko la dunia la simu kutoka kwa Apple na makampuni mengine ya simu. Hadi tunaandika makala hii bado Huawei wanashika nafasi ya pili kwenye biashara ya simu janja.

huawei kukosa playstore

Simu za Huawei kukosa Google Playstore: Mfumo mzima wa Google Play services ndio mfumo mama wa huduma mbalimbali za Google, na kwa kutumia mfumo huu watengenezaji simu wanapata masasisho na maboresho mbalimbali moja kwa moja kutoka Google

Mtazamo wa vitengo vya usalama na pia mtazamo wa kisiasa wa Marekani umekuwa dhidi ya Huawei kwa muda mrefu sana. Wakiamini kampuni hiyo ina mahusiano ya karibu sana na serikali na jeshi la China na hivyo kuwa na uwezekano wa kutumia vifaa na teknolojia zake kwa matumizi ya kijasusi.

INAYOHUSIANA  Instagram Lite Sasa Yaanza Kupatikana.

Ni malalamiko ambayo hadi leo hayajawahi kutolewa ushahidi dhabiti wa hilo kufanyika, na ata Huawei wamekana kwa muda mrefu sana wakisema hawawezi kufanya hivyo kwani utakuwa ni uamuzi utakaoharibu biashara yao kabisa.

Ata mataifa rafiki ya Marekani kama vile Uiengereza wanapata wakati mgumu kuungana na Marekani katika shutuma dhidi ya Huawei – kwa kuwa tayari Huawei wanatengeneza teknolojia na vifaa vya mawasiliano vyenye ubora na kwa bei nafuu.

Maamuzi ya Rais Trump kuweka kampuni ya Huawei katika orodha ya ‘Entity List’ – kuna maana hakuna kampuni yeyote ya kimarekani inayoweza kufanya kazi na Huawei bila ruhusa kutoka serikali ya nchi hiyo. 

INAYOHUSIANA  Post Picha Moja Instagram Ikiwa Imegawanyika Katika Vipande Tisa (9)! #Android #iOs

Kutokana na hilo mahusiano katika ya Huawei na Google yameathirika kama ifuatavyo;

  • Google hawezi kumpatia Huawei huduma za vifaa au programu, wanaweza kumpatia programu ambazo zina leseni ambayo sio ya mauzo/biashara (open source licences).
  • Android ni programu endeshaji inayopatikana ndani ya leseni ambayo si ya mauzo, na hivyo Huawei bado ataweza kuipata.
  • Ila toleo la Android linalotumika kwa sasa kwa Huawei na simu nyingi, ni toleo la kibiashara, hii ni baada ya Google kuongezea vitu vingine mbalimbali hii ikiwa ni pamoja na soko la Google Playstore na apps zingine nyingi za huduma za Google.

Kwa ufupi;

  • Bado Huawei ataweza kuja na simu za Android – kupitia toleo la AOSP (Toleo linalokosa apps nyingi za huduma za Google – Maps, Playstore, Photos, Drive, na nyingine nyingi) na hili linaweza kuwapoteza baadhi ya watumiaji
  • Huawei atakosa kuwa kwenye mfumo wa updates/masasisho ya simu zake mpya na zamani – ambazo huwa zinapata masasisho kupitia mfumo wa Google
  • Kama unatumia tayari simu ya Huawei apps hizo zitaendelea kufanya kazi kama kawaida
  • Masasisho ya OS yako yanaweza yakachelewa sana kuliko kawaida
INAYOHUSIANA  Fanya Simu Yako Ya Android Au iOS Itaje Jina La Mpigaji, Ukipigiwa!

Wiki kadhaa nyuma tulisharipoti kuhusu Huawei kumiliki programu endeshaji nyingine, inasemekana walishaanza kufanya majaribio ya programu endeshaji yao wenyewe ili kujiepusha na matatizo kama maamuzi kama haya yatafanywa na serikali ya Marekani.

Hadi sasa hakuna taarifa nyingi kuhusu programu endeshaji hiyo, ila kwa kiasi kikubwa inaweza ikawa nayo inatengenezwa kwa kutumia Android – kwani ni vigumu kuja na programu endeshaji mpya kabisa kwa kuwa ni vigumu kuwafanya watengenezaji apps kuanza utengenezaji wa apps kwa programu endeshaji nyingine kwa wakati huu.

Je unadhani Huawei wataathirika sana na maamuzi haya ya Marekani? Tayari wamekuwa namba mbili kimauzo, nyuma ya Samsung ila wamekuwa wanapanda kwa kasi na wengi waliamini ndani ya miaka miwili wanaweza kumtoa Samsung nafasi ya kwanza kwenye biashara ya simu.

Facebook Comments

Sambaza
Share.

About Author

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili. | mhariri@teknokona.com |