Simu za Xiaomi zinarekodi data za mamilioni ya watumiaji wake, hicho ndicho kilichosemwa na ripoti mpya kutoka kwa mtafiti wa mambo ya kiusalama.
Xiaomi ni moja ya kampuni ya bidhaa za kielektroniki inayokua kwa kasi zaidi duniani, tena ikinufaika pia kutokana na kikwazo cha Huawei kutumia huduma za Google. Simu za Xiaomi zinashika nafasi ya nne kwenye soko la simu duniani kote, zikiwa nyuma ya Apple, Samsung na Huawei.

Mtafiti wa mambo ya kiusalama, Bwana Gabi Cirlig ametambulisha matokeo ya utafiti wake kwa vyombo mbalimbali vikubwa duniani.
Kinachotokea ni nini?
> Data za kivinjari/browser
Amedai kupitia simu yake ya Redmi Note 8 amekugundua data zote zinazohusiana na tovuti anazotembelea au vitu anavyotafuta kwenye tovuti za utafutaji kama Google zote hutumwa kwenda kwenye vituo vya data (servers) za Xiaomi. Uchunguzi wake umeonesha data hizo zinatumwa kwenda Urusi na China.
> Vitu unavyofanya kwenye mafaili
Pia data nyingine inayotumwa ni pamoja na kuonesha ni mafaili (pamoja na folders) unayafungua kwenye simu yako.
Simu hizo zinarekodi na kutuma data kuhusu tovuti unazotembelea ata ukiingia kupitia ‘Incognito’.

Google, Firefox nao pia huwa wanarekodi data, je kipi ni tofauti?
Kwanza kabisa, hii ni mara ya kwanza kwa ufuatiliaji wa data kufanywa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya kutengeneza simu.
Pili, Google, Apple na makampuni mengine ya Ulaya na Marekani yanasimamiwa na sheria kali za usalama wa data za watumiaji kuhakikisha data zinazorekodiwa si data zinazoweza kumtambua mtumiaji husika wa simu, na pia zinakuwa kwenye usalama mkubwa sana.
Mtafiti Cirlig amedai kitu kibaya kuhusu data zinazorekodiwa na Xiaomi ni pamoja na data kuzidi mipaka ya kuweza kumtambua mtumiaji husika. Na pia data hizo zinasafirishwa kupitia usalama mdogo sana, aliweza kufanya udukuzi wa kuzifahamu data husika ndani ya dakika chache tuu.
Hii inamaanisha ni rahisi kwa wadukuzi kudukua data hizo kutoka kwa Xiaomi na kumtambua mtumiaji husika wa simu.
Xiaomi wamesemaje?
Xiaomi wamejitetea kwa kusema utafiti huo hauko sahihi. Wamesema wanachukulia suala la usalama wa data kwa ukubwa na mapana yake, na pia wanafanya kazi zao kwa kusimama kwenye sheria za ulinzi wa data wa mataifa mbalimbali.