Kampuni ya Samsung imeendelea kuvunja rekodi ya faida katika mapato yake kwa robo ya mwaka ya pili mfululizo katika muongozo wa mapato ya robo ya tatu ya mwaka.
Samsung imesema katika taarifa yake leo kwamba kwa kipindi cha kutoka mwezi Julai hadi mwezi Septemba imepata faida ya kiasi cha dola za kimarekani 12.8 bilioni, katika kipindi kama hiki mwaka jana kampuni hiyo ilipata faida ya kiasi cha dola za kimarekani 4.6 bilioni. Pia kampuni hii imeona mapato yake ama mauzo yake yamepanda kwa karibu 30% kufikia dola za kimarekani 54.7 bilioni.
Je ni biashara ipi iliyowapa Samsung faida hii?!
Ingawa Samsung Electronics Co inajulikana zaidi kwa utengenezaji wa simu za mkononi lakini mafanikio haya inasemekana ni kwa sababu ya biashara yake ya utengenezaji wa chip zinazotumiwa katika mitandao na vifaa vingine. Uhitaji wa chip hizi umeongezeka katika siku za karibuni na kupelekea Samsung kuwaondoa Intel Corp katika nafasi ya kwanza kama mtengenezaji mkubwa, hili limefanya mapato ya Samsung kuongezeka kwa kasi.
Kampuni hii ilipatwa na msala wa simu zake za Galaxy Note 7 kuwa zinalipuka jambo lililopelekea hasara kubwa inaonekana ni wazi kwamba kwa sasa imerudi katika ushindani na makampuni mengine ya simu. Kwetu sisi watumiaji wa simu kampuni hii inapozidi kuimarika kwetu ni habari njema maana tunategemea watakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa matoleo bora zaidi ya simu zao.