Kwa miaka kadhaa wanateknolojia wamekuwa wakijaribu kutengeneza roboti mbalimbali ambazo zitaweza kufanya mambo kadhaa ambayo binadamu anayafanya.
Kila ambaye ameingia katika mchakato huu amejaribu kufanya jambo tofauti lakini haikuwahi kutokea taifa lolote duniani kumpatia hadhi ya Uraia roboti yeyote.
Saudi Arabia imeingia katika vichwa vya habari vya mitandao mbali mbali ya teknolojia baada ya kutangaza uamuzi wake wa kumpatia roboti hadhi ya uraia wa nchi hiyo. Hatua hii imepokelewa kwa mitazamo tofauti tofauti na wadau mbalimbali wa teknolojia.
Roboti huyu aliyepewa jina la Sofia ametengenezwa kwa hasa kutumia Artificial Intelligence (AI) na uwezo wa mashine kujifunza tabia za biandamu, mambo ambayo yanamfanya awe na tabia zinazokaribiana sana na tabia za binadamu wa kawaida. Pamoja na yote anaweza kushiriki majibizano na watu tofauti kama ambavyo binadamu hufanya.
Sofia alipewa taarifa hizo akiwa katika mkutano wa wawekezaji uliofanyika huko Riyadhi mji mkuu wa Saudia. Na alipoulizwa juu ya taarifa hii Sofia hakusita kuonesha furaha yake na shukurani kwa Utawala wa Saudi Arabia.
Wakosoaji wameiona hatua hii kama ni unafiki tu hasa ukizingatia bado kuna watu wengi ambao wanatamani kuwa na uraia wa Saudia lakini hawapati na wapo raia kadhaa wa Saudia ambao wapo hatarini kupoteza uraia kwa sababu ya kuvunja sheria ambazo zinaonekana ni kali kwa baadhi ya watu.
Itazame video ya mahojiano baina ya mwendesha mkutano na Sophia katika mkutano ambao Sophia alitaarifiwa juu ya maamuzi ya Saudi Arabia.