Moja kati ya kampuni mpya mpya katika utengenezaji wa simu, OnePlus, kutoka nchini Uchina waingia rasmi kwneye soko la simu la nchini Marekani.
OnePlus waingia rasmi kwenye soko la simu Marekani baada ya kuingia mkataba na mtandao wa simu wa T-Mobile pamoja na kampuni nguli katika utengenezaji wa vipuri mama vya simu ya nchini Marekani ya Qualcomm.
OnePlus wamejikita zaidi katika kutengeneza simu zenye uwezo wa hali ya juu, na hivyo si za bei nafuu sana lakini unapata simu yenye uwezo mkubwa sana na huku ikiwa ni ya bei ya chini kidogo ukilinganisha na simu zenye sifa/uwezo wa kulingana nazo kutoka makampuni kama Samsung, Huawei au LG.
OnePlus wamefanikiwa jambo hili katika kipindi ambacho kisiasa na kiuchumi kuna vikwazo kadhaa vya kibiashara na kiusalama vinavyowekwa na serikali za Marekani na Uchina dhidi ya biashara za pande nyingine.
Ni hivi karibuni tuu makampuni mengine ya mitandao ya simu nchini humo, AT&T na Verizon, ilibidi wavunje makubaliano ya kibiashara ya kufanya kazi na kampuni ya simu ya Huawei kwa sababu ya katazo la kiusalama kutoka serikali ya Marekani.
Qualcomm ni moja ya kampuni kubwa na kongwe zaidi katika biashara ya kipuri mama za simu. Kampuni ya OnePlus tayari imekuwa ni mteja wa 3 kwa ukubwa wa mahitaji ya vipuri vya Qualcomm, nyumba ya Samsung na LG – kulingana na data za shirika la Canalys.
Mengine machache ya kufahamu kuhusu OnePlus na Qualcomm;
- Bei ya simu zake: wastani wa zaidi ya Tsh. 1,000,000 na zaidi.
- Wapenzi wakubwa wa simu zake ni watu wanaofahamu sifa za simu, na upendelea uwezo wa simu kuliko majina ya simu.
- Ina wafanyakazi takribani 1,000. Katika hao ni wafanyakazi chini ya 400 ndio wanausika na sekta ya mauzo, zaidi ya nusu uhusika na ubunifu na utafiti.
- Maamuzi ya Apple, Samsung, na Huawei kuzidi kuwekeza katika chip za kwao wenyewe kumeifanya kampuni ya Qualcomm kuhakikisha wana mahusiano mazuri na makampuni yanayofanya vizuri kama OnePlus
- Kupitia vipuri kutoka Qualcomm, OnePlus wanategemea kuwa moja kati ya watengenezaji simu wa kwanza kabisa kuingiza sokoni simu zenye sifa na uwezo wa 5G