Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeweka hadharani namba za simu zinazotumiwa zaidi na matapeli kwa njia ya mtandao na kuwasihi wananchi kutotuma pesa kwa watu wasiowafahamu.
Namba hizo ziliwekwa wazi na Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Namba ambazo alizitaja kwamba ndio zimekuwa zikitumika sana ni 0758 713 746, 0764 581 220 na 0744 105 579.
Aidha, jeshi la polisi kwa kushirikiana na kampuni za mawasiliano zimekuwa zikituma ujumbe kwa wananchi kuwatahadhalisha juu ya utapeli wa mtandaoni.
Moja ya ujumbe kutoka Jeshi la polisi ni huu, “Mwananchi, Usikubali kutapeliwa. Usitume pesa kwa mtu usiyemfahamu. Hakiki ujumbe na simu inayokutaka utume pesa. JESHI LA POLISI LINAZINGATIA USALAMA WA PESA ZAKO“.