Tarehe 26 na 27 mwezi Oktoba itabaki katika historia ya Tehama hapa Tanzania kama ndiyo siku wataalamu wa Tehama walianza kukutana na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
Mkutano huu ambao uliandaliwa na kuendeshwa na kamisheni ya Tehama Tanzania ulikua ndio mkutano wa kwanza kuwakutanisha wataalamu wa tehama.
Mkutano huu ulibeba maada kuu ya “Kujenga Uchumi wa Viwanda wa Kidigitali wa Tanzania” na kwa ufupi mkutano huu ulikua unalenga kuwaleta wataalamu wa Tehama pamoja katika ujenzi wa uchumi wa viwanda wa kidigitali kwa Tanzania.
Pamoja na maada kuu mkutano huu ulijadili maada mbalimbali ndogo ndogo, ambazo kwa pamoja zilikua zinaleta mantiki ya maada kuu ya mkutano. Maada hizo ndogo ndogo ni kama zifuatazo;-
Kanuni za Utoaji vibali na utambuzi wa utaalamu wa Tehama.
Katika maada hii wataalamu wa tehama walijadiri umuhimu wa misingi na kanuni za utoaji wa vibali pamoja na utambuzi wa Wataalamu wa Tehama.
Imani na ujasiri katika uchumi wa viwanda wa kidigitali
Katika maada hii mkutano mkuu ulijadili teknolojia zilizopo katika mambo ya usalama wa mitandao, na pia ni mambo yapi hasa wataalamu wa tehama wanatakiwa kufanya ili kuongeza imani kwa watumiaji wa mitandao na mifumo ya Tehama.
Changamoto na Fursa zinazokuja na teknolojia mpya
Hapa mkutano ulijadiri namna ambavyo teknolojia mpya zinaweza kuleta fursa mbali mbali ikiwamo kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa. Mkutano ulijadiri teknolojia mpya mbali mbali zikiwamo pesa za kidigitali na mengineyo.
Majiji janja katika zama za uchumi wa viwanda wa kidigitali.
Mkutano pia ulipata nafasi ya kujadiri namna ambavyo sera za utawala za Majiji kama Dar es salaam zinavyoweza kubadilishwa ili kuweza kuruhusu ubunifu na ukuaji wa teknolojia. Pia mkutano ulijadiri majukumu ya sekta nyingine katika kuboresha huduma za majiji.
Ajira na fursa za ujasiriamali katika Tehama.
Mkutano pia ulijadiri juu ya Ajira na fursa za ujasiriamali katika Tehama, wajumbe waliachambua namna ambayo Tehama inaweza kutengeneza ajira zaidi na kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Mkutano huu ulihitimishwa baada ya kufanyika kwa siku mbili mfululizo na ukishuhudia wataalamu wa Tehama zaidi ya 300 kutoka katika sekta mbalimbali za serikali na za binafsi, pia mkutano huu ulihudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka katika taasisi kubwa duniani kama vile ITU (Umoja wa sekta ya mawasiliano) ORACLE ambayo ni kampuni kubwa katika sekta ya tehama na wengine wengi.