Kama unafuatilia habari basi utakuwa umekutana na taarifa za wafanyakazi kadhaa na mkurugenzi wa Vodacom kushikiliwa na polisi. Baada ya kusomewa mashtaka rasmi, imeonekana sababu kuu inaangukia kwenye utumiaji wa kifaa cha teknolojia na mapato.
Inadaiwa wafanyakazi hao wameshikiliwa na polisi na kupelekwa mahakamani kutokana na agizo la shirika la usimamizi wa mawasiliano la TCRA, kikubwa ni kwamba kuna uwezekano wa utumiaji mbaya wa madaraka uliosababisha upotevu wa mapato kwa serikali/TCRA.
“Vodacom itaendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka za usimamizi”– Sehemu ya taarifa kutoka Vodacom baada ya kupatwa na sakata hili.
Vodacom wanaongoza kwenye sekta ya mawasiliano ya simu Tanzania, na kwa muda mrefu inafahamika ya kwamba ndio shirika la simu lenye mapato mazuri zaidi nchini. Mkurugenzi wa Vodacom, Bwana Hisham Hendi, ameidhinishwa mwezi uliopita tuu kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa miezi kadhaa sasa.

Katika watu wanaoshikiliwa katika kesi hii inahusisha wakuu wa vitengo vya fedha, mapato, sheria na mauzo wote kutoka Vodacom Tanzania. Inasemekana kati ya mwezi Januari na Machi mwaka jana waliingiza kifaa cha mawasiliano ya kimataifa na kuanza kukitumia bila kuwa na leseni ya TCRA.
Kifaa hicho kiliwawezesha kupata namba za kimataifa na kuweza kuzitumia nchini bila kupitia mfumo rasmi unaotambulika. Kifaa kinaenda kwa jina la Proliant ML1 Gen 9 Server (Pabx Virtual Machine).

Baadhi ya makosa.
- Kuingiza, kutumia na kisimika vifaa vya mawasiliano kinyume na sheria
- Kugawa namba za masafa bila kuwa na leseni
- Kumiliki vifaa kilaghai
- Kuisababishia serikali hasara
- Kutumia namba ya simu bila kuthibitishwa na TCRA na kuruhusu mawasiliano ya kimataifa kuingia nchini
- Kutumia kifaa cha mawasiliano ambacho hakiasajiliwa nchini wala kupata idhini ya kutoka TCRA
- Kuisababishia TCRA na serikali hasara ya Tsh. bilioni 5.25.
Vodacom wamesema huduma yao haitaathirika kwa namna yoyote katika kipindi hiki. Shirika la TCRA limewekeza vizuri katika teknolojia za kisasa za usimamizi wa mitandao ya simu na inawezekana kamata hii imetokana na teknolojia hizo.
Vyanzo: TheCitizen, Mwananchi, Bloomberg