Wikiendi iliyopita kulikuwa na uzinduzi wa kitabu cha Riwaya jijini Dar es Salaam. Jina la kitabu linaenda kwa jina la Mimi na Rais. Hadi sasa unaweza ukawa unajiuliza kwa nini tuandike kuhusu kitabu katika kona ya teknolojia?
Si hivyo, kitu kikubwa ambacho kimevutia ni historia iliyotolewa iliyohusisha mambo kadhaa ya mtandaoni ambayo yaliweza kufanikisha hadi uwepo wa uzinduzi huu wa kitabu cha mwandishi Lello Mmassy.
Hongera @LelloMmassy kwa kuzindua kitabu cha @MimiNaRais! Kazi kwetu wapenzi wa Riwaya! pic.twitter.com/BqMQf2bP99
— PAT?? (@PatNanyaro) July 13, 2019
Kwanza uzinduzi wa kitabu ulifanyika katika moja ya kumbi ya moja ya kampuni nguli katika masuala ya teknolojia za kidigitali – SmartCodes, na asilimia kubwa ya waliofika katika uzinduzi huo ni vijana walio maarufu kwenye mitandao ya kijamii – hasa hasa Twitter na pia kama mimi ni watu ambao tupo katika kazi zinazohusisha utumiaji wa mitandao.
Amini, si kawaida kuwa na watu wanaotoka sekta hii katika uzinduzi wa bidhaa ambayo siyo ya kimtandao/kiteknolojia – hapa ikiwa ni kitabu.

Umaarufu na mafanikio ya kimtandao ya uzinduzi wa kitabu hiki umetokana na juhudi za mwandishi kusambaza sehemu ya stori hii wakati anaiandika mtandaoni. Na kundi la wapenzi wa kazi zake waliweza kusambaza zaidi na hivyo kupata idadi kubwa ya watu waliokuwa wakifuatilia kila wiki kupitia mitandao ya kijamii – Twitter, Facebook na Telegram.
Katika kuonesha ya kwamba mafanikio haya yamechangiwa sana na watu walio kwenye mitandao ya kijamii hasa hasa Twitter, mwandishi Lello Masy ameishukuru jamii ya kitanzania inayotumia mtandao wa Twitter. Pongezi za ziada zikiendi kwa kijana Kennedy Mmari – ambaye kupitia kampuni yake ya Serengeti Bytes alijitolea kuanza kuhariri matoleo ya wiki ya riwaya hii yaliyokuwa yakitolewa kipindi cha mwanzo wa mwaka. Serengeti Bytes hawakuishia hapo tuu bali ndio waliosimamia uchapaji na uandaaji wa uzinduzi wa kitabu cha riwaya hii.
Teknokona inatoa pongezi wa Lello Mmassy na bwana Kennedy kwa kuwa mfano mzuri wa mafanikio yanayoweza kuonekana pale vijana wanapoungana na kutumia mitandao ya kijamii kwa faida zao binafsi na ata kwa jamii kwa ujumla.