Bing kuzidi kukua. Tovuti namba mbili katika huduma ya utafutaji ya Bing itazidi kujikita na kukua katika eneo la utafutaji kwa watumiaji wa kompyuta.
Haya yamesemwa na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Microsoft inayomiliki Bing, Bwana Satya Nadella.

Huduma ya Bing ni ya pili nyuma ya Google, katika huduma za utafutaji (Search).
Bwana Satya amesema haya siku chache baada ya kampuni ya Apple kuvunja mkataba na Bing uliokuwa unahakikisha mtandao huo unatoa huduma za utafutaji katika app ya Siri inayopatikana kwenye simu na kompyuta za Apple – iPhones, iPad na MacBook.
Apple wameipatia huduma ya utafutaji ya Google dili hili, vifaa vya Apple vina maelfu ya watumiaji duniani kote na hivyo mkataba huu ni muhimu kwani unahakikishia huduma ya utafutaji uhakika wa kutumika.
Mitandao ya utafutaji kama vile Google na Bing inapata mapata yake kupitia matangazo mbalimbali yanayowekwa katika matokeo ya utafutaji. Hivyo kila huduma inavyotumiwa zaidi ndivyo inavyotengeneza pesa zaidi.
Huduma ya Bing imekuwa ikitumika katika matokeo ya kimtandao ya app ya Siri na Spotlght katika Mac tokeo mwaka 2013.
Katika ripoti ya kimapato waliyoiweka wazi hivi karibuni inaonesha mapato yake ya Bing yamekuwa yakikua kwa asilimia nane katika kipindi cha mwaka mmoja. Kuna uwezekano yakaathirika na uamuzi Apple, ingawa mkurugenzi wake anasema hawataathirika.