Marubani wafanya makosa mengi katika kipindi cha mwaka mmoja na lawama zimeelekezwa kwenye janga la Covid 19. Tokea mwezi Mei mwaka jana hadi kipindi hichi makampuni mengi ya ndege yamepunguza safari zake kutokana na kuwa na abiria wachache.
Suala hili limesababisha marubani wengi kuwa kazini mara chache sana kuliko kawaida. Kuna marubani wanaojikuta nyumbani kwa kipindi cha miezi kadhaa kabla ya safari nyingine, na hili linasababisha matatizo.
Matatizo yaliyojitokeza hivi karibani
- Kuna rubani aliyesahau kuondoa breki ya ndege wakati ndege inavutwa na kigari cha kusaidia kupanga ndege. Tukio hili lilisababisha uharibifu wa kigari hicho.
- Kuna rubani ilimbidi kurudia jaribio la kutua ndege mara tatu, wakati katika hali ya kawaida tayari yeye ni rubani mzuri na huwa anaweza kutua vizuri ndege bila kuzidi majaribio mawili.
- Kuna ofisa mwengine/rubani msaidizi alisahau kuwasha mifumo ya kuzuia vifaa muhimu vya mawasiliano vya ndege vilivyo maeneo ya nje kuganda (kutokana na baridi kali lililo kwenye anga za juu).. Ilikuwa ni bahati tuu ndege hiyo kufika salama bila kupata tatizo.
Watafiti wengi wa sekta hiyo wamesema ni kawaida kwa marubani ambao wanakaa bila kuendesha ndege kwa muda wa miezi kadhaa kusahau baadhi ya mamb0 muhimu yanayohakikisha usalama wa ndege na abiria.
Aprili na Mei mwaka jana kwa Marekani tuu, usafiri wa ndege ulikuwa chini kwa zaidi ya asilimia 75 ukilinganisha na kipindi cha kabla ya Korona. Katika miezi hii ya hivi karibani hali imekuwa nzuri lakini bado ipo chini, inasemekana asilimia za safari ni kama asilimia 43 ya kabla ya janga hilo.
Septemba 15, nchini Indonesia ndege ya Airbus 330 ilipoteza muelekeo ikiwa inatua katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kualanamu, hali ya kutokuwa kazini kwa muda mrefu kwa rubani na wafanyakazi wa kituo cha kuongoza ndege ilichukuliwa kama chanzo kikubwa cha ajali hiyo. Rubani alikuwa ameendesha ndege kwa muda usiozidi masaa 3 katika kipindi cha siku 90 kabla ya ajali hiyo, wakati msaidizi wake hakuwa amefanya kazi katika kipindi miezi 3.
Janga la Covid 19 limesababisha kwa miezi mingi safari za anga kuwa katika kiwango kidogo kabisa duniani. Hali hii imesababisha maelfu ya ndege kutotumika na hivyo marubani wake kujikuta wakiwa kwenye likizo ndefu.
Vyanzo: Los Angeles Times na vingine mbalimbali
No Comment! Be the first one.