Ukiwa mtumiaji wa kompyuta na hasa kama shughuli zako ili kwenda vizuri na kukamilika bila tabu unahitaji kifaaa hicho cha kielektroniki basi huna budi kufahamu mengi ambayo yatakufanya uwe huru bila ya kutegemea mtu mwingine kukusaidia kitu fulani mathalani kulinda faili ndani ya Windows 7, 8, 10.
Mara baada ya kuweka hewani makala inayohusu jinsi ya kuweka nenosiri kwenye nyaraka mmoja wa wasomaji wetu akauliza swali lililosababisha kufikiria kuandaa somo hili kwa faida ya wengi. Aliuliza inawezekana kuweka ulinzi kwenye faili kwenye kompyuta inayotumia programu endeshi-Windows 7? Jibu la swali hilo ni ndio lakini itabidi kutumia programu ya nje kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.
Sasa wataalamu wa masuala ya teknolojia tunafahamu kuwa zipo programu kadha wa kadha ambazo zinaweza kufanya hiyo kazi mfano Folder Guard, AxCrypt na nyingine nyingi tuu. Kati ya hizo zote ambazo hata watu wengi wametoa maoni mazuri lakini ambayo binafsi nimeshawahi kuitumia kwa miaka kadhaa na nikaipenda ni AxCrypt.
Kitu ambacho programu wezeshi-AxCrypt inafanya ni kuwezesha mtumiaji kuweka nywila kwenye faili kuweza kufikia vilivyomo ndani. Hatua ya kwanza kabisa ni kutembelea tovuti ya kampuni iliyotengenza AxCrypt ili kuweza kupakua programu husika kulingana na aina ya programu endeshi (iwapo ni 32 bit au 64 bit).
Hatua ya pili mara baada ya kuhakikisha AxCrypt ipo kwenye kompyuta ni kwenda kwenye faili ambalo unataka kulinga kisha bofya kitufe cha upande kwenye kipanye halafu chagua AxCrypt > Encrypt. Andika nywila unayotaka kisha irudie tena bila kubadilisha herufi/tarakimu ulizoweka mara ya kwanza kisha bonyeza OK.
Kama wewe ni msahaulifu wa vitu vidogo vidogo kama nenosiri unaweza ukachagua kompyuta ikimbuke nyiwila uliyoweka ili utakapokuja kufungua tena isikudai kitu kama hicho kwa kuweka alama kwenye kipengele cha kwanza (inaonekana pichani) au hilo ndio liwe nenosiri kwa mafaili mengine utakayopenda kuyafunga-weka alama kwenye chauo la pili ingawa si njia nzuri kuitumia kwa sababu za kiusalama.
