Korea Kaskazini wakana kuiba kwa kutumia udukuzi. Serikali ya Korea Kaskazini imekana shutuma ya kuhusika na wizi wa zaidi ya dola bilioni 2 za Kimarekani kwa njia ya mtandao.
Ripoti ya Umoja wa Kimataifa (UN) iliyovuja mwezi uliopita iliitaji Korea Kaskazini kuhusika na udukuzi wa njia ya mtandao dhidi ya mabenki na tovuti za pesa za njia ya mtandao (Crypto) na kuondoka na pesa zenye thamani ya zaidi ya Tsh trilioni 4.6 (Dola Bilioni 2 za Marekani).

Ripoti hiyo ilidai pesa hiyo ilitumika katika ununuaji wa silaha mbalimbali za kivita – hii ikiwa ni pamoja na zile zilizopigwa marufuku.
Serikali ya Korea Kaskazini imesema shutuma hizo si za kweli na inachukulia kama vita ya kipropaganda inayofanywa na Marekani pamoja na washirika wake ikilenga kutafuta sababu ya taifa hilo kupewa vikwazo zaidi.
Korea Kaskazini imekuwa ikishutumiwa sana siku hizi ya kwamba huwa inajihusisha na udukuaji wa huduma mbalimbali za kifedha kwa lengo la kujipatia pesa za kigeni ili kufanikisha manunuzi ya baadhi ya vitu ambavyo ni vigumu wao kupata kwa sasa kutokana na taifa hilo lenye usiri mkubwa kuwa chini ya vikwazo mbalimbali vya kibiashara na vya kisiasa.