Simu za Tecno Spark zimekuwa kwenye midomo ya watu kutokana na sababu mbalimbali lakini hasa kwa kuziboresha kwa kuwa na muonekano wa kiushindani bila kusahau nguvu ya betri inayowekwa.
Miezi kadhaa nyuma ilitoka Tecno Spark Power 2 Air na ingawa si mpenzi wa rununu zinazobeba jina hilo nikavutiwa kutaka kuifahamu kiundani bidhaa husika kwanini imekuwa ikiongelewa sana sehemu nyingi duniani. Sifa zake ni kama ifuatavyo:-
Kipuri mama/Muonekano
Simu janja hii ina urefu wa inchi 7 huku ung’avu/ubora wa picha ukiwa wa kawaida (720p+/kwenye Netflix picha zitaonekana vizuri tuu) huku ufanisi wake wa kazi ukibebwa na MediaTek Helio A22 kama kipuri mama.
Uwezo wa betri
Simu janja nyingi wengi wetu tunazichukia kutokana na betri kuishiwa na chaji haraka hivyo kuhitaji kuwa kwenye umeme kwa zaidi ya mara moja ndani ya siku moja. Simu hii ina 6000mAh; saa 15 ukiwa unatumia kutazama picha jongefu au saa 13 iwapo utaitumia kucheza magemu. Kuhusu teknolojia ya kuchaji haraka bado haijafahamika.
Kamera
Ubora/uwezo wa kamera kwenye simu hii ni kamera moja mbele ikiwa na MP 8+taa mbili (zile picha gizani ambazo mtu anajipiga mwenyewe zitaonekana murua). Upande wa nyuma zipo tatu; kubwa ina MP 13 ikifuatiwa na mbili zenye MP 2 halafu ile ya mwisho ni mahususi kwa ajili ya utambuzi wa vitu (AI)+taa ya mwangaza.

Memori/Bei na Mengineyo
Tecno Spark Power 2 Air ina GB 32 pamoja na kuweza kukubali memori ya ziada mpaka GB 256, RAM ni GB 3. Bei yake ni $115|zaidi ya Tsh. 264,500 bei ya ughaibuni. Vilevile, ina spika mbili, teknolojia ya kutumia alama ya kidole, kadi mbili za simu, LTE na VoLTE kwenye kasi ya intaneti, sehemu ya kuchomeka spika za masikioni, Bluetooth 5.0.
TeknoKona imeshakufahamisha undani wa rununu husika sasa kazi ipo kwako kuamua iwapo inakufaa na kukufanya na wewe uwe mmojawapo uliyevutiwa na kuinunua simu hiyo.
Chanzo: GSMArena
No Comment! Be the first one.