Teknolojia ya vioo ya Gorilla Glass ndio teknolojia inayotumika zaidi katika ‘display’ za simu, tableti na vifaa vingine janja ili kuepusha kuvunjika pale vinapodondoka.

Kampuni inayotengeneza vioo hivyo, Corning, imekuja na toleo jipya linalosemekana kuwa ni salama zaidi. Kampuni hiyo ya jijini New York nchini Marekani inadai vioo vyake hivi vipya vya Gorilla Glass vinanguvu ya zaidi ya mara nne ukilinganisha na vya wapinzani wake.
Inasemekana teknolojia ya Gorilla Glass inatumika katika zaidi ya vifaa bilioni 4.5 tokea mwaka 2007, wateja wakuu wa kampuni hiyo ya Corning ni pamoja Samsung, Apple, Motorola, LG, HP na makampuni mengine.
Inasemekana kwa toleo hili la 5 la Gorilla Glass basi uwezekano wa simu kutovunjika kioo pale ikidondoshwa kutoka umbali wa mabega au kiuno cha mtumiaji hadi chini unakuwa mkubwa sana..pia ni vigumu zaidi kioo kukwanguliwa na kitu.

Data kutoka utafiti mmoja wa kimataifa unaonesha ya kwamba takribani asilimia 85 ya watumiaji wa simu janja washaangusha simu janja zao angalau mara moja kwa kipindi cha mwaka mmoja….na asilimia 55 washaangusha kwa mara tatu au zaidi kwa kipindi hicho hicho.
Inategemewa muda si mrefu simu janja za hadhi ya juu kutoka makampuni makubwa zitakuja na toleo hili la kisasa la Gorilla Glass.
Je wewe unakubali ya kwamba kuvunjika kwa vioo vya simu ni moja kati ya tatizo kubwa zaidi kwa wamiliki wa simu janja? Unachukua hatua gani kuhakikisha simu yako inaendelea kuwa salama?
Chanzo: BBC, DenverPost