Google wanataka kuzidi kutawala eneo la kiofisi. Google Jamboard ni ubao wa kisasa wenye uwezo wa kushirikisha ufanyaji kazi kwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Ata ujio wa kompyuta bado haujaondoa uitaji wa kuwa na ubao katika maofisi, ubao unatumika kwa ajili ya vipindi vya kutafuta mawazo mapya ya kibiashara au kikazi – ‘brainstorm’, unatumika kuandikia ratiba mbalimbali, na kazi nyingine nyingi tuu.
Google Jamboard ni ubao janja unaolenga kurahisisha kabisa majukumu ya utumiaji wa ubao. Ubao huu utahakikisha watu wote wenye wazo flani wanaweza kuchangia kwa kuandika kwenye ubao huo ata kama wapo nje ya ofisi – moja kwa moja kupitia app ya simu za mkononi.
Ubao huu kutoka Google unategemewa kuingia sokoni muda wowote kuanzia sasa na inaonekana moja kwa moja unalenga kuleta ushindani dhidi ya kifaa kutoka Microsoft kinachofahamika kwa jina la Microsoft Surface Hub (Bofya kusoma uchambuzi wake).
Kikubwa kinachotofautisha Google Jamboard dhidi ya Microsoft Surface Hub ni kwamba Jamboard ipo rahisi sana kutumika na pia ni bei nafuu zaidi. Microsoft Surface Hub ni kompyuta kamili wakati Jamboard ni moja kwa moja ni ubao – sema tuu ni wa kisasa na umeboreshwa kwa teknolojia rahisi za kurahisisha ushirikiano baina ya watumiaji.
Sifa zake kwa uchache;
- Uwezo wa kuandika kitu kwa kutumia peni spesheli (stylus) na kufuta kwa kutumia ufutio au ata kwa kutumia kidole chako tuu
- Pia watumiaji mbalimbali wanaweza shiriki kwenye kinachoendelea kwenye ubao huo kupitia app za android na iOS kwenye simu au tableti.
- Mwenye ubao huo anaweza alika watu kushiriki kwa urahisi na kupitia kamera ya ubao huo pamoja na spika zake basi vikao vinaweza fanyika kwa urahisi tuu (huduma ya kuchati kwa video na sauti ya Google Hangout inapatikana).
- Ubao huu inauwezo wa kutumia zingine nyingi za Google kama vile Google Maps na Docs moja kwa moja kwenye ubao huo.
- Unaweza andika kwa mwandiko mbaya na ubao huu utaweza kuubadilisha mwandiko huo kwenda kwenye mwandiko uupendao wa kikompyuta zaidi.
- Pia kila kinachoandikwa kwenye ubao huo kinahifadhiwa moja kwa moja kwenye huduma ya Google Drive na hivyo ni vigumu sana watu kupoteza data juu ya kile mnachokifanya kwenye ubao huu. Pia inakuja na teknolojia za HDMI 2.0, USB Type C, na USB 3.0.
Bei?
Ubao huu janja kutoka Google utauzwa kwa dola 6000 za Marekani, takribani Tsh milioni 12 hivi. Ila kama teknolojia nyingi mpya tunategemea bei ya vifaa kama hivi zitashuka huko mbeleni.