Google Drive na Google Photos zatenganishwa na Google. Google wamefanya uamuzi huo wakisema unatokana na maoni ya utumiaji ambao wamekuwa wanasema muunganiko wa huduma hizo umekuwa ukiwachanganya.
Google wamesema kuanzia mwezi wa saba huduma hizo zitakuwa tofauti rasmi. Muda mrefu imekuwa picha zinazohifadhiwa kwenye huduma ya Google Photos zimekuwa zikichukua nafasi kwenye Google Drive.
Watumiaji wengi wameona ni bora huduma za picha ziwe tofauti na zile za Google Drive kwa kuwa wamekuwa wakitumia huduma ya Google Drive kwa ajili ya uhifadhi wa mafaili zaidi na hivyo inaleta usumbufu pale wanapoweka programu ya Google Drive Backup and Sync kwenye kompyuta kwani programu hiyo udownload hadi picha ambazo wao hawakuwa na kazi nazo: walitaka kutumia mafaili tuu.
Picha na video zako ambazo tayari zipo kwenye Google Photos hazitaathirika na mabadiliko haya. Tayari Google wamesema pia wanafanyia kazi uwepo wa eneo la kuchagua kuweka picha kwenye Google Photos kutoka Google Drive, chaguo ambalo litaitwa ‘Upload from Drive’, huduma hii itaingizwa ndani ya Google Photos.
Kwa ufupi:
- Picha na video mpya utakazoweka kwenye Google Drive hazitaonekana kwenye Google Photos
- Pia picha mpya na video utakazoweka kwenye Google Photos hazitaonekana kwenye Google Drive
- Ukifuta picha kwenye Google Drive haitafutika kwenye Google Photos
- Kama una picha hiyo kwenye Google Drive ata ukiifuta kwenye Google Photos haitaondoka kwenye Google Drive
Google wamesema ila ingawa kutakuwa na utofauti huo bado kiwango cha data (MB/GB) kimahesabu kitakuwa ni kimoja. Kumbuka kuupload picha za kawaida kwenye Google Photos ni bure, zinachukua nafasi zako za ujazo wa Google Drive kama ni picha za mafaili makubwa sana – ila kwa picha za kawaida za kutumia simu moja kwa moja Google wanakuwekea kwenye ubora unaokidhi sifa ya uhifadhi wa bure.