Google wanategemea kuja na maboresha makubwa ya kimuonekano na utendaji katika huduma yao ya barua pepe ya Gmail. Moja ya uwezo unaotegemewa ni mtu kuweza kutuma barua pepe zinazofutika baada ya muda flani.
Maboresho ya kimuonekano yanakuja kwenye huduma mbalimbali za Google, hii ikiwa ni pamoja na huduma zingine kama vile Google Calendar, Google Keep, Google Tasks na zinginezo.
Gmail Confidential Mode
Google wameleta kitu kinaitwa ‘confidential mode’ ndani ya huduma ya barua pepe ya Gmail. Kama barua unayotuma ukaichagulia pangilio/setting hii basi barua pepe yako itatumwa ikiwa na sifa kadhaa;
Mtu atakayeipokea atashindwa kuituma kwa mwingine (forward). kuidownload. wala kucopy vitu vilivyokwenye barua pepe hii.
Mtumaji barua pepe inayokuwa katika mfumo wa ‘confidential mode’ anaweza iwekea tarehe ya kujifuta huko inakoenda (expiration date), pia anaweza kuchagua uwezo wa kufanya barua pepe hiyo isiweze kufunguka hadi umpatie anayeipokea code (itakayotumwa kwako kwa njia ya sms pale mtu atakapotaka kuifungua barua pepe uliyomtumia).
Je itakuwaje kama mtu akiwa anatumia huduma ya Gmail kwa njia zingine nje ya kwenda mtandao wa Gmail au kutumia app ya Gmail?
- Kama mtu anatumia njia ya kupokea barua pepe zake kwa njia za POP/IMAP/SMTP, akitumiwa barua pepe yenye sifa ya Confidential Mode hataipata barua pepe hiyo kikamilifu, bali atapata ujumbe utakaomtaka kuifungua barua pepe hiyo kwenye kivinjari/browser.
- Atapokea barua pepe yenye ujumbe unaosema ‘Ujumbe/Barua pepe hii imetumwa kwa njia ya Gmail Confidential Mode, unaweza kuusoma kwa kubofya hapa’
Google wamesema muonekano mpya, ambao tunaamini utakuja na uwezo huu kwa Gmail, utaanza kupatikana kwa baadhi ya watumiaji wake ndani ya wiki chache kuanzia sasa.
Je unadhani wazo hili ni zuri sana? Tupe maoni yako na usisahau kushare makala hii na wengine.
Gmail: www.gmail.com