Biashara ya vifaa vya kieletroniki hususani simu janja pamoja na ukuaji wa teknolojia kwa kuwepo kwa aina mbalimbali za upashanaji habari lakini bila kusahau ushindani baina ya makampuni vitu vyote hivi ndio vinazalisha fununu kuhusu uzinduzi, bei, lini itaingia sokoni.
Mwaka huu Apple wanatazamia kutoa iPhone toleo la 12 zitakazotofautiana katika vipengele kadha wa kadha na kutokana na janga la virusi vya Corona huenda uzinduzi ukafanyika mwezi tofauti na ilivyo zoeleka. Hata hivyo, tayari taarifa kuhusu bei ya simu hizo zimeshafahamika ingawa si rasmi lakini waswahili husema “Lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja“.
Ndio, kati ya mwezi Oktoba-Novemba mwaka huu tutaweza kufahamu sifa rasmi za iPhone 12 mbalimbali kuanzia yenye uwezo mdogo hadi ile ya juu kabisa na bei zake zinaweza zikakushangaza kidogo kama ni mtu ambae umekuwwa ukifuatilia toleo mbalimbali za iPhone.
iPhone 12/iPhone 12 Max
Nimependa kuanza kwa mtiririko wa simu janja ndogo kwenda kubwa kulingana na majina yaliyopewa. Sasa iPhone 12 inaaminika kuwa itauzwa $649|zaidi ya Tsh. 1,492,700, kioo chake kina urefu wa inchi 5.4 huku ile yenye inchi 6.1 (inaaminika kuwa iPhone 12 Max) yenyewe ni $749|zaidi ya Tsh. 1,722,700, RAM GB 4 kwa zote mbili.
iPhone 12 Pro/iPhone 12 Pro Max
Kwenye iPhone 12 Pro kioo chake kinategemewa kuwa inchi 6.1 Super Retina XDR OLED, RAM GB 6 na bei yake ikianzia $1,049|zaidi ya Tsh. 2,412,700 kwa bei ya ughaibuni. iPhone 12 Pro Max itakuwa na kioo chenye urefu wa inchi 6.7, RAM GB 6 huku ikianza kuuzwa kwa $1,149|zaidi ya Tsh. 2,642,700.

Hao ndio Apple na bidhaa zao ambapo kuna mengi ambayo hayajawekwa wazi lakini iwapo unategemea kununua toleo lijalo basi ujipange vyema kifedha.
Vyanzo: Tom’s guide, TechRadar