Flutterwave yafungiwa nchini Kenya ikipewa shutuma ya kutumiwa katika utakasishaji fedha. Flutterwave ni huduma ya utumaji malipo iliyofanikiwa zaidi barani Afrika.
Flutterwave inasaidia kufanikisha malipo kwa uharaka kwa biashara kubwa na ndogo kutoka nchi moja kwenda nyingine. Kupitia kutumia huduma ya Flutterwave biashara moja inaweza kufanya malipo kwa uharaka zaidi kwenda kwenye akaunti ya biashara iliyo kwenye taifa jingine barani Afrika. Inarahisisha pia biashara za nje ya Afrika kupokea au kufanya malipo kwenda kwa biashara iliyo barani Afrika.
Kufikia Februari mwaka huu, kampuni ya Flutterwave ilikuwa na thamani ya dola bilioni 3.
Tatizo lipo wapi Kenya?
Shirika la Kiserikali la Urejeshaji Mali la nchini Kenya kupitia mahakama limefunga akaunti za Flutterwave na za wateja wake kadhaa likitaka kujiridhisha kama miamala kadhaa yenye hofu nayo imetoka sehemu salama na kwa malipo halali. Wanaamini vyanzo vya malipo na jinsi pesa hizo zilivyotoka kupitia Flutterwave, kwenda kwenye akaunti za wapokeaje, kuna utakasaji pesa unahusika.
Kutakasisha pesa – ni njia ya kupata fedha ambazo si halali, kwa kuzitafutia njia za kuzihalalisha, mfano kuzigeuza mapato halali kutoka vyanzo visivyo vya kweli.
Kiasi cha zaidi ya Shilingi za Kenya Bilioni 6.2 ( Zaidi ya Tsh Bilioni 122) zilizokwenye akaunti 62 katika mebenki kadhaa nchini humo zimefungiwa. Pesa hizo ni kwenye akaunti ya Flutterwave na akaunti zingine 4 za wateja wao (waliopokea malipo).
Inasemekana pesa hizo zilitumwa kutoka mataifa kadhaa, zikaingia kwenye akaunti ya Flutterwave kabla ya kulipwa kwenda kwenye akaunti za benki za makampuni mengine 6. Kitengo cha Uchunguzi kinataka kujiridhisha kwa kufahamu vyanzo vya pesa hizo – zililipwa kutoka kwa watu gani, na kwa kazi gani.
Flutterwave wanasemaje?
Flutterwave wamekanusha kuhusika kwa namna yeyote na kitendo chochote cha utakasaji pesa. Wanasema wanatumia makampuni yenye sifa na hadhi ya juu katika kuhakiki mihamala yao.
Shirika la Urejeshaji Mali linataka kutaifisha pesa zote zinazohusishwa katika sakata hili. Jambo hili linaweza kuchukua miezi kadhaa kutatuliwa, katika kipindi chote hicho wateja wa Flutterwave itawabidi watafute suruhisho jingine kwa malipo ya uharaka.
Tutaendelea kufuatilia muendelezo wa suala hili.
Vyanzo: TechCrunch na vyanzo mbalimbali
No Comment! Be the first one.