Je unaweza unaweza kufikiri ni vigumu Facebook kufahamu pale watumiaji wake wanapofanya ngono? Imefahamika si vigumu, na yote yanafanikishwa kupitia mifumo ya data za apps na huduma za matangazo ya Facebook.
Shirika linalotetea haki za watu dhidi ya teknolojia za kisasa – Privacy International limetoa ripoti inayoonesha tovuti maarufu ya mtandao wa kijamii ya Facebook kwamba huwa unataka kufahamu hadi maisha ya kingono ya watumiaji wake ili kutumia data hizo kwenye huduma zake za kimatangazo.
Apps za uzazi na kufuatilia mizunguko ya hedhi ni maarufu sana hasa hasa kwa wanawake. Ripoti ya Privacy International inaonesha kupitia teknolojia zake za kimatangazo za Facebook zinazowekwa kwenye apps hizo baadhi ya apps maarufu zimekuwa zikituma (kushare) taarifa za watumiaji wake na hali zao hii ikiwa ni pamoja na masuala ya ngono kwenda huduma ya matangazo na data ya Facebook.
Apps za masuala ya uzazi na kufuatilia mizunguko ya hedhi zimekuwa zikihitaji data/taarifa mbalimbali kutoka kwa mtumiaji ili kuweza kutoa ushauri mzuri zaidi kwa mtumiaji. Baadhi ya data hizo zinahusisha tarehe za mizunguko ya hedhi, na pia kama mwanamke anataka ujauzito basi atakuwa anapata ushauri wa siku za kufanya ngono na yeye kukubali (kutick) au kukataa kama tendo hilo halilifanya – kwa kuweka taarifa hiyo kwenye app hizo.
Apps maarufu zilizokutwa zikifanya hivyo ni pamoja na
-
- Maya kutoka kwa Plackal Tech (ina zaidi ya downloads milioni 5 kwenye Google Play),
- MIA kutoka kwa Mobapp Development Limited (downloads milioni 1) na
- My Period Tracker iliyotengenezwa na Linchpin Health (downloads zaidi milioni 1 Google Play)
Uchunguzi wa Privacy International umekuta data hizo huwa zinatumwa kwenda kwa baadhi ya makampuni ya kimatangazo na hii ikiwa ni pamoja na Facebook. Iwapo mtumiaji amejiunga kwenye app husika kwa kutumia Facebook (login with Facebook) basi Facebook wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kumtumia mtumiaji huyo matangazo pale atakapokuwa anatumia huduma za Facebook au za washirika wa Facebook kupitia kurushiwa matangazo yanayohusiana na maisha yake ya kingono kwa wakati huo.
Suala hili ni uvunjifu wa sheria mbalimbali za kimataifa katika mabara ya Ulaya na ata Marekani. Inasemekana muda si mrefu Facebook wanaweza jikuta katika mashtaka kutoka vyombo vya Marekani, Uingereza na Bara la Ulaya (EU).
Suala la ‘Big Data’ – mjumuhisho wa data/taarifa mbalimbali za watumiaji wa intaneti limekuwa changamoto sana kwa sasa. Suala kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuhakikisha data za watumiaji wa huduma/mitandao/apps mbalimbali zinakuwa salama na haziendi kutumika nje ya matakwa yao.