Ergonomics ni taaluma ya kisayansi inayohusika na uelewa wa mwingiliano uliopo kati ya binadamu na mashine au mifumo. Ergonomics inahusika na usalama, faraja, urahisi wa matumizi na utendaji uliopo katika mazingira ya kazi. Wataalamu wa Ergonomics wanatumia kanuni, nadharia na data mbalimbali kuboresha mifumo ya ufanyaji kazi wa mashine ili kukuza uzalishaji na kupunguza makosa ya kibinadamu kazini.
Kuna mchanganyiko wa taaluma nyingi ndani ya Ergonomics kama vile saikolojia, uhandisi, uzoefu wa mtumiaji na nyingine nyingi. Kupitia Ergonomics watengenezaji wa bidhaa mbaimbali huzingatia ukubwa wa mwili wa mtu binafsi, nguvu, ujuzi, kasi, uwezo wa kuona na kusikia katika utengenezaji wa bidhaa zao.
Kuna aina tatu za Ergonomics ambazo ni Ergonomics ya kimwili, Ergonomics ya utambuzi na Ergonomics ya shirika. Katika Ergonomics ya kimwili hii huhusika na uhusiano uliopo kati ya mwili wa binadamu na mazingira yake ya kazi mfano kiti anachokalia kazini, meza anayotumia kazini, kazi zote ngumu anazofanya pamoja na kuinua vitu vizito. Madhara ya kutozingatia Ergonomics ya kimwili katika mazingira ya kazi ni pamoja na maumivu ya shingo, mabega, mgongo, macho, kifua, misuli kukaza, mwili kuuma, maumivu ya kiuno na mengine mengi.
Ergonomics ya Utambuzi huhusika na ufanyaji wa michakato ya kiakili kama vile kutambua, kukumbuka na kujenga hoja. Ergonomics ya utambuzi husaidia kupunguza mzigo wa kazi katika kufikiria, katika kufanya maamuzi na katika utendajikazi wenye ustadi.
Ergonomics ya shirika huhusika na uandaaji mzuri wa mazingira ya kazi kwa wafanyakazi ili wasipatwe na kero wala maumivu yoyote katika ufanyaji kazi wao. Hii ni pamoja na upangaji wa muda wa kazi, kushirikiana katika kazi ngumu na kupata muda wa kutosha wa kupumzika baada ya kazi.
Ergonomics ina Faida zifuatazo:
- Wafanyakazi kutopata maumivu wakati wa kazi
- Kuongezeka kwa uzalishaji
- Uhudhuriaji mzuri wa wafanyakazi kazini kutokana na kuwa na afya njema.
- Kuongezeka kwa mapato ya kampuni kutokana na ufanisi wa kazi utakaokuwa ukifanyika.
- Huondoa hatari zilizopo katika mazingira ya kazi.
No Comment! Be the first one.