Google wamesema kivinjari chao cha Chrome kupunguza utumiaji wa RAM kwa kiasi kikubwa katika toleo jipya la kivinjari hicho. Google wamesema kuna maboresho kadhaa waliyofanya kwenye teknolojia inayoendesha kivinjari hichi maarufu.
Katika toleo la Chrome la namba 89 wamesema wanaonufaika zaidi ni watumiaji wa Windows 10 na faida hiyo ikionekana pia kwa watumiaji wa programu endeshaji zingine.

Katika toleo la Windows 10 Google wamesema kwa sasa Chrome itapunguza utumiaji wa RAM kwa hadi asilimia 22 zaidi.
Kuna mabadiliko gani?
Kwa sasa Chrome itapunguza utumiaji mkubwa wa RAM kwa tab ambazo hazitumiki kwenye Chrome, na kuruhusu tab inayotumika kwa muda huo ndio kuweza kupata ruhusa ya kutumia RAM kwa kasi ya kawaida. Wanasema kuna uwezekano wa kuokoa zaidi ya nafasi ya MB 100 ya RAM kwa kila tab ambayo haitumiki kwa wakati husika.
Kwa watumiaji wa simu za Android Google wamesema kwa sasa kutakuwa na unafuu wa asilimia 5 katika utumiaji wa RAM, lakini pia ufanisi/uharaka wa ufungukaji wa app ya Chrome utaongezeka kwa zaidi ya asilimia 7, na huku kurasa zikifunguka kwa haraka zaidi kwa asilimia 2.
Kwa watumiaji wa simu janja za kisasa za Android zenye RAM ya kuanzia GB 8 Google wamesema watapata toleo la Chrome la familia ya bit 64, na wataweza kuona ongezeko la kurasa/website kufunguka kwa uharaka wa asilimia 8.5 zaidi, na huku urahisi wa kushusha na kupandisha kurasa ukiwa bora zaidi kwa asilimia 28 (scrolling).
Kwa muda mrefu kumekuwa na shutuma dhidi ya kivinjari cha Chrome ya kwamba kinatumia RAM kwa kiwango kikubwa sana hasa hasa kwenye kompyuta. Hivyo tusishangae kuona Google wanazidi kuwekeza katika kuifanya Chrome kuwa na ufanisi ulio bora zaidi.
No Comment! Be the first one.