Inafahamika ulimwenguni kote kwamba BlackBerry wameachana na utengenezaji wa simu janja lakini wameendelea kutoa huduma mbalimbali zinazohusisha programu mbalimbali zinazosaidia kwenye masuala ya ulinzi kwenye ulimwengu huu wa teknolojia.
Polepole BlackBerry imekuwa ikiuza hakimiliki zake kwenye vitu ambavyo inavimiki kwa makampuni mbalimbali na hivi karibuni imeuza umiliki wake ambao una thamani ya $600 milioni|zaidi ya Tsh. 1.3 trilioni kwenda kwa Catapult IP Innovations kampuni iliyoundwa mahususi kabisa kushikilia hakimiliki ya vitu mbalimbali vya BlackBerry.
BlackBerry ni moja ya waundaji wa mapema zaidi kwenye teknolojia ya kutuma jumbe kwa njia ya mtandao pamoja na vitu vingine vya thamani zaidi kwenye dunia ya leo huku ikielezwa inashikilia hakimiliki (patents) ya vitu vyenye thamani kati ya $2-3 bilioni au hata kuweza kufikia $4-5 bilioni kama vitauzwa kwa kupigwa mnada.
Kutokana na kutofanya vizuri kwenye biashara ya simu janja mwaka 2020 BlackBerry ilijiweka kando kwenye upande huo na ushindani lakiniimeendelea kuwaangalia wateja wake wanaolipia huduma fulani za kiusalama kwa ajili ya shughuli zao na hata mauzo ya $600 milioni ambapo $450 milioni zimelipwa hapo hapo na $150 milioni zitalipwa kwa makubaliano ya ahadi. Hata hivyo, bado BlackBerry imebaki na uwezo wa kuja kuzitumia hakimiliki zake na wateja wake hawataathiriwa na hicho ambacho kimefanyika ingawa baadhi ya wafanyakazi wa BlackBerry watahamia Catapult.
Mpango huo bado haujakamilika vizuri kwani serikali ya Canada itabidi kuyapitia makubaliano hayo ili kujiridhisha kuwa suala hilo la kununua hakimiliki za BlackBerry si hatari kwa usalama wa taifa. Hatua hiyo inafanyika kutokana na kwamba Third Eye Capital ya Toronto-Canada iliisaidia Catapult fedha za kuweza kununua umiliki huo kutoka kwa BlackBerry.
Vyanzo: GSMArena, mitandao mbalimbali
No Comment! Be the first one.