Kuna mambo mengi ambayo muasisi wa kampuni ya Apple alisema kamwe kampuni hiyo haitakuja kuyafanya ila sasa yanafanyika na kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayochangia mafanikio mapya ya kampuni hiyo kimauzo. Katika tukio lao spesheli jijini San Francisco nchini Marekani Apple wametambulisha simu mpya, iPad na kifaa kinachofahamika kama Apple TV.
Hapa fahamu yote mapya kuhusu simu zao mpya zitakazoanza kupatikana mapema mwishoni mwa mwezi huu wa tisa.
“Zinaonekana sawa tuu na matoleo yaliyopita, ila ukweli ni kwamba tumebadilisha kila kitu kwenye iPhone hizi mpya” – Tim Cook
Simu hizi zinakuja na prosesa mpya kabisa kutoka Apple inayofahamika kama A9, wenyewe wanadai prosesa hii inafanya kazi kwa kasi zaidi kwa zaidi ya asilimia 70% ukilinganisha na ile iliyokuwa katika toleo la iPhone lililopita.
Kimtazamo wa haraka haraka simu hizi zinaonekana sawa na zile zile zilizopita, yaani iPhone 6 na iPhone 6 Plus lakini ndani ndipo kuna maboresho makubwa zaidi kiteknolojia. Ukubwa wa umbo ni ule ule, iPhone 6S ni inchi 4.7 na iPhone 6S Plus ni inchi 5.5
Maboresho ya kamera
Kamera imeboreshwa zaidi, wakati iPhone 6 zilikuwa na kamera ya MegaPixel 8 hizi iPhone 6S zitakuja na kamera ya MegaPixel 12. Pia kamera za simu hizi mpya zinauwezo wa kupiga video za kiwango cha ubora wa juu zaidi cha 4K, kwenye iPhone zilizopita kiwango kilikuwa ni 1080p HD.
Unapenda selfi?
Kwa wapenda picha za selfi basi kuna habari nzuri, kioo chako cha Retina kitakuwa kinatoa mwanga mkali zaidi pale utakapokuwa unajipiga picha za selfi katika maeneo yenye giza au mwanga mdogo.
3D Touch
Kioo cha simu hizi kimoboreshwa kikija na teknolojia ya 3D Touch (Teknolojia ya miguso) ambayo itafanya aina tofauti tofauti za miguso pale unapogusa apps zikupe majibu tofauti.
Rangi
iPhone 6S na 6S Plus zitakuja katika rangi za dhahabu, bati na majivu. Pia kuna nyongeza moja ya rangi ya dhahabu spesheli ifahamikayo kama ‘rose gold metallic’.
Diski Uhifadhi (Storage)
Bado ukubwa wa diski uhifadhi unazokuja nao ni ule ule, kutakuwa na matoleo ya GB 16, GB 64 na GB 128.
iOS 9
Programu endeshaji, zinakuja na toleo jipya kabisa la iOS, iOS 9. Watumiaji wengine wa simu na tableti za Apple wajiandae kuweza kusasisha (upgrade) kuanzia tarehe 16 mwezi huu wa tisa.
Soma Pia – Mambo Ambayo Steve Jobs Alisema Kamwe Apple Hawatayafanya na Wanayafanya Sasa!
Simu hizi zitaanza kupatikana tarehe 12 mwezi huu wa tisa katika baadhi ya nchi na kuendelea kusambaa katika mataifa mengine. Bei bado haijatangazwa rasmi na ikifahamika tuu tutaiweka hapa, endelea kutembelea TeknoKona. Nini maoni yako kuhusu simu hizi mpya za iPhone?
No Comment! Be the first one.