AlterEgo. Watafiti wa Chuo cha MIT cha nchini Marekani wamekuja na teknolojia ya kuweza kutambua maneno unayoyasema hata pale ambapo katika hali ya kawaida hayasikiki – kwa kuwa haujaongea.
Chuo cha MIT kinasifika sana kwa tafiti na ubunifu unaokuja kuwa na faida kubwa kimaendeleo na kiuchumi nchini humo.
Utafiti huu unaokwenda kwa jina la AlterEgo, umetengeneza kifaa kinachohitaji kuvaliwa pembeni ya kichwa na kugusa eneo la nyuma la sikio; upande wa pembeni ya taya, na chini kidogo ya mdomo (lips).
Kifaa hicho kinasikiliza kwa makini mifumo ya mawasiliano ya neva (neuromuscular signals). Kwa kuwa tayari wanasayansi wameweza kuainisha aina ya tabia za neva na mwenendo wa mdomo (lips) pale ambapo maneno yanasemwa – yaani hata kama ni kutamkwa maneno kwa kiwango ambacho macho ya kawaida ya mwanadamu hayaoni kama mdomo wa mtu umesogea.
Kifaa hiki kitaweza kutambua tabia za neva na kitendo cha mdomo kuchezacheza ambapo kwa macho ya kawaida huwezi kuona.
Kwenye upande wa kifaa hiki kukupa majibu au taarifa, eneo la kifaa linalogusa nyuma ya sikio lako kuna uwezo wa kukuwasilisha ujumbe kwenda kwenye sikio lako kwa njia ya kutetemeka (vibration) – wewe utasikia sauti kamili. Mfumo huu wa headphones unahakikisha ya kwamba unaweza bado kusikia vitu mbalimbali vya kawaida kwa kuwa mfumo huu hauzibi tundu la sikio.
Mfumo mzima unatumia teknolojia ya akili isiyo ya kweli kwenye kikompyuta – AI / Artificial Intelligence. Kifaa hiki ni ‘Kifaa janja’ kinachoweza kupata taarifa unazozisoma, au kuiambia kompyuta yake ifanye (mfano mahesabu) na wewe kupata majibu ya moja kwa moja — mambo yote haya yakifanyika bila mfumo huo kutengeneza kelele/sauti yoyote kusikika.
Katika majaribio kwa sasa kinauwezo wa kupokea maswali yako na kukupatia data zinazohusu masuala kama vile hali ya hewa, kukupa majibu ya mahesabu kupitia njia hiyo hiyo, kuweka kumbukumbu za kalenda na nyingine ndogo ndogo kama hizo.
Utumiaji wa baadae;
Tayari watu wanaangalia teknolojia hii na kuona inaweza kuja kutumiwa baadae katika maeneo mbalimbali.
i) Moja ya sehemu muhimu kutumika ni kwa wale wanaofanya kazi katika mazingira yenye kelele sana kama viwanja vya ndege, viwandani, marubani, n.k kwani teknolojia hii itawawezesha kuweka kumbukumbu ya mambo au kuwasiliana na mwingine bila kutumia sauti.
ii) Jeshini. Pia teknolojia hii inaonyesha kuleta maboresho makubwa kwa wanajeshi wanaokwenda kwenye vita spesheli (Special Ops). Katika vita vya namna hii suala la ukimya wakati kazi inaendelea ni muhimu sana – kupitia teknolojia hii wanajeshi wanaweza kuwasiliana na kupeana maelekezo bila kutoa sauti yyyote.
Vipi unaionaje teknolojia hii? Je, unaweza kuona sehemu gani zingine za maisha ya kila siku inaweza kutumika au kuboresha?
Chanzo: MIT