Unazifahamu tovuti zinazotembelewa zaidi duniani? Teknokona leo tunakuletea orodha ya tovuti zinazotembelewa zaidi na watu mbalimbali duniani. Mtandaoni kuna aina mbalimbali za tovuti na kila moja ina nafasi yake katika matumizi ya kila siku kwa watumiaji wa mtandao. Tovuti zinazoongoza kwa kutembelewa sana ni tovuti za kutafutia vitu mtandaoni (Search Engines) na tovuti za mitandao ya kijamii.
Katika 10 bora ya orodha hii ya tovuti zinazotembelewa zaidi duniani tovuti nyingi zinaonekana kuwa ni za mitandao ya kijamii. Mbali na hilo 5 bora ya tovuti hizo ni pamoja na:
Google: Google ni tovuti ya kutafutia taarifa mbalimbali mtandaoni. Kupitia tovuti ya Google unaweza kutafuta kitu na ukaonyeshwa ni tovuti ipi au mtandao upi wa kijamii wenye hicho kitu unachokitafuta. Kwa siku Google hutumika mara bilioni 5.6 kutafuta vitu mtandaoni, na kwa mwezi hutumika mara bilioni 86.9. Hii ndio tovuti inayoongoza duniani kwa kutembelewa sana na watumiaji.
Youtube: Tovuti hii hutumika kuangalizia video, kutiririsha video za mbashara na kutuma video mtandaoni. Tovuti hii ya Youtube imeshika nafasi ya pili kutokana na kuwa na watumiaji wengi wanaoitumia katika mambo mbalimbali. Kwa siku Youtube hutumiwa na watu takriban milioni 122 na kwa mwezi hutumiwa na wastani wa watu bilioni 2.
Facebook: Huu ni mtandao wa kijamii wenye zaidi ya watumiaji bilioni 1 mpaka sasa. Kwa sasa mtandao wa kijamii wa Facebook unamilikiwa na Meta pamoja na mitandao mingine kama WhatsApp na Instagram. Mwaka 2021 Facebook iliripoti kuwa ina takribani watumiaji bilioni 1.9 kwa siku. Facebook imekuwa mtandao wa kijamii wa kwanza kuwa na watembeleaji wengi duniani.

Wikipedia: Hii ni tovuti ya uandishi, uchapishaji na usomaji wa makala mtandaoni. Tovuti hii huwa na makala kuhusu mambo mbalimbali kama bidhaa, watu, kampuni na mambo mengine mengi. Watu hutembelea tovuti hii wanapotaka kujua zaidi kuhusu kitu flani na tovuti hii hubeba taarifa za kuaminika na zenye vielelezo vya chanzo cha taarifa hiyo kwaajili ya ufuatiliaji zaidi.
Yahoo: Hii ni tovuti ya utafutaji wa vitu mtandaoni kama ilivyo Google. Tovuti hii ni ya zamani zaidi na ndio iliyokuwa ikitumika sana na watu kabla ya Google. Kupitia yahoo search unaweza ukapata mambo mbalimbali yaliyopo mtandaoni na kwa sasa Yahoo ina watumiaji takriban milioni 255.
No Comment! Be the first one.